WAWAKILISHI Pekee wa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki timu ya Simba imepangwa kucheza na Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika hatua ya robo Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Simba wataanza kucheza mchezo wao wa kwanza kati ya April 15 au 17 katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar Es Salaam.
Timu nyingine Al Ittihad ya Libya watacheza na ndugu zao Al Ahli Tripoli.
Mtajiri wa Misri Pramids wataanzia nyumbani kucheza na TP Mazembe kutoka DR Congo huku Al Masry ya Misri watacheza na RSB Berkane ya Morocco.
Simba akifanikiwa kumuondoa Orlando Pirates nusu Fainali atacheza na mshindi kati ya Al Ittihad au Al Ahli Tripoli kutoka Libya.
Orlando Pirates wamekuwa na rekodi ya kutoa vipigo kwa timu iwe kubwa au ndogo katika mechi sita za hatua ya makundi wameshinda mechi nne, sare moja huku wakipoteza mchezo mmoja mbele ya Al Itihad Tripoli ya Libya ugenini.
Katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini wababe hao wanashika nafasi ya tano wakiwa na pointi 35 katika mechi 23 walizocheza wakishinda nane, sare 11 na kufungwa michezo minne.
Mabingwa hao wa Klabu Bingwa Afrika 1995 na mabingwa mara tisa wa Ligi Kuu kikosi chao kinaongozwa na Kocha Fadlu Davids, huku wachezaji nyota wakiwa ni straika Bandle Shandu mwenye mabao manne kwenye kombe hilo, Kabelo Dlamini mwenye mabao matatu na Terrence Dzvukamanja aliyefunga mawili.