Featured Kitaifa

SERIKALI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Written by mzalendoeditor

Na Englibert Kayombo WAF- Dodoma

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imelenga kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha zinapatikana hapa nchini na zinakuwa za uhakika na karibu zaidi na maeneo ya wananchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipokuwa akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Afya na Taasisi zake mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

“Lengo letu sio tuu kupunguza gharama za Serikali kulipia Watanzania kwenda nje ya nchi kupata huduma za matibabu, bali pia tunataka huduma hizo zipatikane hapa hapa nchini karibu zaidi na maeneo wanayoishi lakini pia wawe karibu na familia zao waweze kuhudumiwa vizuri” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuhakikisha upatikanaji wa Huduma Bora za Afya kwa wananchi kwa kusogeza Huduma za Ubingwa na Ubingwa bobezi karibu na wananchi wanapoishi kwa kujenga, kupanua na kukarabati Hospitali za Rufaa kuanzia ngazi ya Mikoa hadi Taifa.

Kuhusu hali ya utoaji wa huduma za Kibingwa na Ubingwa Bobezi, Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari 2022, Wizara kupitia hospitali za kitaifa, kanda na hospitali maalum imehudumia jumla ya wagonjwa 3,341,393 kati ya hao wagonjwa wa nje (OPD) walikuwa 3,035,427 na wagonjwa wa kulazwa (IPD) walikuwa 293,680.

Waziri Ummy amesema kuwa Wizara ya Afya inaratibu jumla ya miradi 39 ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Hospitali 8, ukarabati na upanuzi wa Hospitali 31, ambapo utekelezaji wa miradi hiyo umeendelea katika Hospitali za Rufaa za Kanda 4, hospitali maalum moja (1) na Hospitali za rufaa za Mikoa 26.

Waziri Ummy amesema kuwa Wizara imeendelea kutekeleza afua mbalimbali za tiba nchini ambapo katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari, 2022 jumla ya Wagonjwa 21,230,469 walipatiwa huduma, ambapo Wagonjwa 20,428,932 ni wa nje na Wagonjwa 801,537 walilazwa na hivyo kupungua kwa idadi ya Wagonjwa ikilinganishwa na jumla ya Wagonjwa 21,586,217 walipatiwa huduma katika kipindi kama hicho cha Julai 2020 hadi Februari 2021.

Kuhusu upatikanaji wa dawa, Waziri Ummy amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22, kiasi cha shilingi bilioni 200 kilitengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi. Hadi kufikia mwezi Februari 2022, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 119.8 sawa na asilimia 59.9 ya fedha yote iliyotengwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Stanslaus Nyongo ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maendeleo ili Watanzania waweze kupata huduma bora za matibabu hapa hapa nchini.

“Watanzania wanahitaji kutibiwa, na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amepeleka fedha nyingi kwenye upande wa elimu na afya na tumeona hapa tunajenga vituo vya kutolea huduma za afyat tunataka huduma zipelekwe kwa wananchi na pamoja na upatikanaji wa dawa kwa uhakika” amesema Mhe. Nyongo.

Aidha Mheshimiwa Nyongo ameishauri Serikali kulitazama kwa mapana zaidi suala la Bima ya Afya kwa wote na kusema kuwa ndio suluhisho la uhakika wa matibabu kwa Watanzania pamoja na ustahimilivu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)

“Leo tunajenga majengo na huduma zinatolewa na dawa kupelekwa lakini Watanzania wengi bado hawana uwezo wa kulipia gharama za Bima, ipo haja ya sisi Kamati kukaa na Serikali kuishauri vyema zaidi juu ya mustakabari wa Bima ya Afya kwa wote” ameseme Mhe. Nyongo

About the author

mzalendoeditor