Featured Michezo

TANZANIA KUUNGANA NA NCHI ZA SADC KUADHIMISHA SIKU YA UKOMBOZI KUSINI MWA AFRIKA

Written by mzalendoeditor

Na Eleuteri Mangi – WUSM, Dodoma

Serikali ya Tanzania itaungana na Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuadhimisha Siku ya Ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika Machi 23, 2022 wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa Habari machi 22, 2022 jijini Dodoma Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni Dkt. Emmanuel Temu amesema Siku ya Ukombozi ni muhimu kuadhimishwa ili kutoa na kuwapa elimu vijana waweze kujua historia ya nchi zao.

“Waasisi ya wa Taifa letu chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, nchi yetu ilisimama kidete na tulitumia rasilimali zetu kwa hali na mali, nguvu za kidiplomasia na za kijeshi kusaidia mapambano ya vyama vya Ukombozi katika nchi mbalimbali ili kuzisaidia kupata uhuru na utawala na hatimaye haki kupatikana kikamilifu” amesema Dkt. Temu.

Dkt. Temu amesema kuwa wakati wa harakati za ukombozi wa Afrika, Tanzania ilitoa mchango mkubwa katika kusaidia kwa hali na mali harakati za ukombozi katika Bara la Afrika hasa nchi za Kusini mwa Afrika.

Hatua hiyo ilizifanya nchi hizo za kusini mwa Afrika kuichangua Machi 23 kwa kuzingatia siku kama hiyo mwaka 1988 majeshi ya Afrika yalihitimisha Utawala wa kimabavu na ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini katika Mji wa Cuito Cuanavale uliopo Kusini mwa Angola na kuulazimisha utawala wa ubaguzi wa rangi na washirika wao kukubali kuzingatia Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSCR) 435/78 ambalo lilipelekea uhuru wa Namibia.

Katika kuadhimisha siku hiyo, Wizara imepanga kufanya Kongamano katika Shule ya Sekondari ya Kongwa, mkoani Dodoma, mahali ambapo wapigania uhuru wa vyama vya Ukombozi kutoka nchi za Kusini mwa Afrika walitumia muda wao katika kambi kubwa ya Kongwa kupata mafunzo ya Kijeshi ili kuzikomboa nchi zao mikononi mwa wakoloni.

Aidha, shughuli nyingine zitakazofanyika siku hiyo ni pamoja na maonesho ya picha za historia ya Ukombozi na makala, Utoaji wa tuzo na zawadi kwa wanafunzi walioandika insha bora kuhusu mchango wa Tanzania katika Ukombozi wa Afrika pamoja na ziara ya kutembelea kumbukumbu zenye urithi wa Ukombozi zilizopo Kongwa.

Katika kufanikisha harakati za Ukombozi,lugha adhimu ya Taifa Kiswahili ilitumika kama lugha ya Ukombozi ambayo hadi sasa imefanikiwa kuwa lugha ya kazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na hatimaye sasa Kiswahili kimetengewa Julai 7 kila mwaka kuwa ni siku ya Kiswahili Duniani.

Siku ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika iliidhinishwa na Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika Windhoek, nchini Namibia Agosti 2018 na kupitisha mwezi Machi 23 ya kila mwaka kuwa ni siku ya kusherehekea ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika ambayo ni njia ya kuenzi na kuhifadhi historia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

About the author

mzalendoeditor