Featured Kitaifa

LAAC YAISHAURI MSALALA KUONGEZA UMAKINI KATIKA KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO

Written by mzalendoeditor

Na. Asila Twaha Msalala

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC) imeishauri Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 16 Machi, 2022 na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa wakati walipowasili na kupokea taarifa ya utekelezwaji wa miradi inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo ukiwemo Ujenzi wa Jengo la Utawala na Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.

Kufuatia taarifa iliyosomwa na Bw. Ezekiel Zablon (Mchumi wa Msalala Dc) Kamati ilikagua ujenzi wa Jengo la Utawala na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Zedi amesema, upo ucheleweshwaji wakutokumalizika kwa wakati jengo hilo sababu ya watendaji kutokufuatilia ujenzi huo kwa makini na kusababisha ujenzi kutokamilika.

Aidha, Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa iliendelea na ziara yake kwa mradi wa Jengo la Hospitali ya Halmashauri la Wilaya ya Msalala na kubaini kutoshirikishwa kwa wananchi katika suala la uundwaji wa kamati za usimamizi uliosababisha kutofuata taratibu za ununuzi wa vifaa vya ujenzi mpaka vifaa hivyo kusababisha hasara na vyengine kuharibika.

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC) imeshauri uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kuwa makini na ufuatiliaji wa karibu wa miradi yote ya maendeleo na kuutaka kushirikisha wananchi ili kuleta uwazi na uwajibikaji katika utekelezwaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Sophia Mjema imeishukuru Kamati kwa ushauri na maelekezo waliyoyatoa kuyachukua na kushirikiana kwa pamoja na watendaji na kuahidi kusimamia kwa ukaribu na umakini miradi ya maendeleo yote inayotekelezwa katika Mkoa huo.

About the author

mzalendoeditor