Featured Kitaifa

KIPANGA AUTAKA UONGOZI WA MKOA WA SIMIYU KUSIMAMIA VYEMA UJENZI WA CHUO CHA VETA

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (Mb) akikagua eneo la ujenzi wa Chuo cha VETA Mkoa wa Simiyu.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (Mb) akitoa malekezo wakati alipotembelea kukagua ujenzi wa Chuo cha VETA Mkoa wa Simiyu.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (Mb) akifafanua jambo wakati alipotembelea kukagua ujenzi wa Chuo cha VETA Mkoa wa Simiyu.

…………………………..

Na WyEST,SIMIYU

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga ameutaka Uongozi wa Mkoa wa Simiyu kuhakikisha unasimamia vyema na kwa karibu ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kinachojengwa Kata ya Bunamhala mjini Bariadi ili kuhakikisha fedha iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi huo inatumika kama ilivyopangwa.

Ameyasema hayo mkoani Simiyu wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho cha Mkoa ambapo amesisitiza kuwa mradi huo ni wa Serikali na fedha zinazotumika ni za walipa kodi hivyo zinapaswa kulindwa ili kuhakikisha zinatekeleza malengo yaliyowekwa.

“Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kupitia Katibu Tawala hapa, mradi huu ni wa kwenu hivyo ni lazima tuhakikishe tunausimamia kwa ukaribu. Tutengeneze team work kuhakikisha tunasimamia kutoka mwanzo mpaka mwisho ili tuweze kuilinda dhamana tuliyopewa ya fedha za walipa kodi” amesema Mhe. Kipanga.

Naibu Waziri Kipanga amefafanua kuwa Serikali inajenga jumla ya vyuo 25 vya VETA vya Wilaya ambapo katika awamu ya kwanza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alitoa jumla ya Shilingi bilioni 40 za ujenzi wa vyuo hivyo kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.6 kila kimoja.

Ameongeza kuwa Mhe. Rais ametoa fedha nyingine Shilingi bilioni 8 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya zingine nne na bilioni 8 zingine kwa ajili ya ununuzi wa samani za vyuo vyote 29.

“Hivi tunavyozungumza Wilaya 29 tayari kuna vyuo vya VETA ambavyo zaidi ya bilioni 48 .8 imetumika lakini Wilaya zingine vyuo hivyo vilikuwa bado havijakamilika hivyo Mhe. Rais alipopata fedha ya uviko 19 Oktoba mwaka jana alisema vyuo hivyo ni lazima vikamilike na kuanza kutoa huduma,” amefafanua Kipanga.

Awali akisoma taarifa Mwenyekiti wa Kamati ya Utekelezaji wa mradi huo, Bazil Gibson amesema ujenzi wa chuo hicho chenye jumla ya majengo 25 ulianza Februari 2022 na unatarajiwa kukamilika Mei 2022 na kwamba utagharimu jumla ya Shilingi bilioni 5.1 hadi kukamilika.

Amesema chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 500 kwa wakati mmoja ambapo 320 kati yao watakaa bweni na wengine 180 wa kutwa.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Lupakisyo Kapange amemhakikishia Mhe. Kipanga kuwa uongozi wa Wilaya hiyo utausimamia mradi huo ipasavyo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Prisca Kayombo amesema wamefarijika sana na ujenzi wa chuo hicho kwa kuwa wanaamini kitawanufaisha wananchi wa Mkoa huo na kuahidi kuyafanyia kazi ipasavyo maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri huyo.

About the author

mzalendoeditor