Featured Kitaifa

RAIS SAMIA ATOA SH.BILIONI 41 KULIPA MADENI YA WAKANDARASI WA MIRADI YA MAJI NCHINI

Written by mzalendoeditor

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso,akizungumza wakati wa Mkutano wa Wizara ya maji na wadau wa Sekta ya maji  ili kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao kilichofanyika leo Machi 10,2022 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga,akizungumza wakati wa Mkutano wa Wizara ya maji na wadau wa Sekta ya maji uliofanyika  leo Machi 10,2022 jijini Dodoma.

SEHEMU ya washiriki wakifatilia mada mbalimbali wakati wa Mkutano wa Wizara ya maji na wadau wa Sekta ya maji  wenye kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao kilichofanyika leo Machi 10,2022 jijini Dodoma.

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso,akimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga,wakati wa Mkutano wa Wizara ya maji na wadau wa Sekta ya maji wenye lengo la kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao kilichofanyika leo Machi 10,2022 jijini Dodoma.

……………………………………………………

Na Alex Sonna-DODOMA

KUELEKEA wiki ya maji,Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Sh. bilioni 41 kwa ajili ya kulipa madeni ya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maji nchini.

Pia Machi 22 anatarajia kukutana na wadau wa maji wakiwemo wakandarasi Jijini Dar Es Salaam ili kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Hayo ameyasema wakati wa Mkutano wa Wizara ya maji na wadau wa Sekta ya maji  ili kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao kilichofanyika leo Machi 10,2022 jijini Dodoma.

Aweso amesema kuwa tayari serikali imeidhinisha bilioni 41 kwa ajili ya kuwalipa madeni wakandarasa wanaodai kupitia miradi ya maji nchini.

“Hapa napokea taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu Anthony Sanga kuwa tayari Mheshimiwa Rais Samia ameshaidhinisha kiasi cha Sh. bilioni 41 za kulipa wakandarasi  na March 22, Rais Samia  atakutana na wadau wa maji kusikiliza changamoto zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi,”amesema Aweso

Aweso amesema kuwa alipokea malalamiko ya ucheweshaji wa malipo kutoka kwa wakandarasi, Hali ambayo imekuwa ikidhorotesha utekelezaji wa miradi.

“Wakandarasi wanaokamilisha kazi zao wapewe fedha zao kwa wakati badala ya kuchukua muda mrefu kuzifuatilia, suala la uaminifu lina umuhimu mkubwa na kutoa mfano wa mmoja wa wakandarasi Wilaya ya Handeni ambaye alilipwa Sh600 milioni lakini haifanyi kazi,”amesisitiza 

Aweso amesema Mkutano huo ni muhimu kwa kuwa umebeba maudhui ya kuboresha ushirikiano baina ya Wizara na wadau hao hali itakayosaidia miradi ya maji Nchini kutekelezwa kwa uwazi na uwajibikaji .

“Tujenge utaratibu wa kuzungumza na wakandarasi Kila mwaka,hii itasaidia kuibua changamoto nyingi ambazo zitapata nafasi ya kutatuliwa na hatimaye kuondokana kabisa na uhaba wa maji,”amesema

Aidha Aweso amewataka wasambazaji wa vifaa vya ujenzi wa miradi ya maji kuacha unyonge na kuhofia kutosikilizwa na Serikali na badala yake wahakikishe wanafuata ngazi huhisika za uongozi kabla ya kupeleka tenda.

“Wadau wetu msiwe wanyonge,msikubali kunyonywa ,hii wizara ina ngazi nyingi za uongozi,hakikisheni tenda zote mnazopata zinapitia kwa wahusika ili kuondoa mkanganyiko uliopo,acheni kufuatia njia za panya zinawaponza mnakosa haki yenu,”ameeleza Aweso.

Nao baadhi ya wadau wa sekta ya maji wameeleza changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wao kuwa wamekuwa wakisumbuliwa wanapofuatilia malipo yao hivyo kuiomba Serikali kupitia wizara hiyo kuona haja ya kufuatilia suala hilo ili walipwe kwa wakati na kujiendeleza kiuchumi.

Akiongea mwa niaba ya wengine,mmoja wa wadau hao Isabella Mapunda kutoka Kampuni ya Mama Mapunda General Supply amesema wakandarasi wengi wanaotekeleza miradi ya maji sio waaminifu kwani wanakwamisha juhudi za wadau Katika kutatua kero ya maji .

“Tunadharauliwa, tunapeleka vifaa Lakini hatulipwi kwa wakati ,tunazungushwa sana,tunapoanza kufatilia malipo yetu wanatujibu kuwa malipo yetu bado hayajakailika,wakati wahusika Wakuu wanateleza kuwa tayari fedha imeingia,”amesema

About the author

mzalendoeditor