Featured Kitaifa

WANAWAKE WA KIISLAMU WATAKIWA KUTUMIA AKILI NA MAARIFA ILI KUJIENDELEZA KIUCHUMI

Written by mzalendoeditor
Sheikh wa Mkoa wa Dodoma Alhaj Mustafa Rajab Shaban,akizungumza wakati  akifungua kongamano la wanawake wa Kiislamu mkoani Dodoma. 
Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda, akizungumza baada ya kuzinduliwa kwa kongamano la wanawake wa Kiislamu mkoani Dodoma. 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) Mkoa wa Dodoma Bi. Fatma Mwasa akizungumza baada ya kuzinduliwa kwa kongamano la wanawake wa Kiislamu mkoani Dodoma. 
……………………………………………………….
Na Bolgas Odilo-DODOMA
Sheikh wa Mkoa wa Dodoma Alhaj Mustafa Rajab Shabab,amewataka wanawake wa Kiislamu kutumia akili na maarifa ili kujiendeleza kiuchumi katika kuwaletea maendeleo yao bila kusubiri kuwezeshwa.
Kauli hiyo ameitoa jijini Dodoma wakati akifungua  kongamano la wanawake wa Kiislamu mkoani Dodoma.
“Sio lazima kusubiri mpaka muwezeshwe, nyinyi wenyewe mnaweza kufanya kazi yeyote halali na mkajiingizia kipato pasipo kuwezeshwa.
“Zamani mwanamke alikuwa anaonekana kama mtu ambaye hawezi kufanya lolote la kuleta maendeleo, ila kwa sasa hiyo dhana haipo, mnaweza bila kuwezeshwa,” alisema kwa msisitizo Sheikh Rajab.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda alihimiza ushirikiano kwa wanawake wote wa Kiislamu na kuwataka watoto wa kike kujikita kwenye elimu zote ya dunia na ya kidini.
Munkunda alisema kuwa, kwa kufanya hivyo kutawasaidia kujifunza mengi na kufanya mambo makubwa ikiwemo kushika nyadhifa mbalimbali katika jamii kwa ujumla.
“Sasa hivi ni wakati wa kushirikiana ili tufanye makubwa zaidi, bila ushirikiano hatuwezi kuendelea mbele zaidi.
“Tuhakikishe watoto wetu wanapata elimu zote, ya dini na dunia ili waweze kuongeza ujuzi na maarifa kwa ajili ya kupata maendeleo binafsi.
“Wanawake tunaweza kushika nyadhifa mbalimbali, hivyo tusikatishwe tamaa,” alisema Munkunda.
Aidha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) Mkoa wa Dodoma Bi. Fatma Mwasa aliahidi kuwasomesha baadhi ya wanafunzi wa kike katika vyuo vya ufundi stadi VETA ili kuwaongezea ujuzi na maarifa.

About the author

mzalendoeditor