Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na Balozi wa Sweden nchini Tanzania mheshimiwa Anders Sjöberg,mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 7 Machi 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Sweden nchini Tanzania mheshimiwa Anders Sjöberg,mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 7 Machi 2022.
……………………………………………………………..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 7 Machi 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sweden nchini Tanzania mheshimiwa Anders Sjöberg,mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Katika mazungumzo hayo Balozi Sjöberg amemkabidhi Makamu wa Rais mualiko rasmi wa serikali ya Sweden kwa Tanzania katika kushiriki mkutano wa kimataifa wa mazingira ukiadhimisha miaka 50 ya tamko la pamoja la uhifadhi wa mazingira lililofanyika Stockholm nchini Sweden mwaka 1972. Amesema mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha viongozi wa wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa mbalimbali duniani ili kujadili kwa pamoja namna ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira ambao ni tishio kwa dunia hivi sasa.
Balozi Sjöberg ameipongeza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi thabiti katika uhifadhi wa mazingira pamoja na kutenga maeneo maalum ya upandaji miti na hifadhi za mazingira. Amesema katika kukabiliana na changamoto za mazingira ushiriki wa pamoja unahitajika baina ya mataifa ili kupunguza athari za uharibifu wa mazingira zinazojitokeza hivi sasa.
Ameongeza kwamba Tanzania na Sweden zinaendelea kushirikiana katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya kuendeleza nishati mbadala pamoja na uhifadhi mazingira kama vile kushirikiana na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kwa kuwajengea uwezo watumishi katika usimamizi wa sheria za mazingira.
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele katika kuhifadhi mazingira kwa kutambua kwamba athari za uharibifu wa mazingira madhara yake ni makubwa kwa wananchi ikiwemo ukosefu wa mvua zinazochagiza kilimo na ufugaji hapa nchini. Amesema ni muhimu kwa mataifa yalioendelea katika teknolojia kushirikiana na Tanzania katika kutumia teknolojia rahisi kupata nishati mbadala ya gharama nafuu itakayotumiwa na wananchi ili kulinda mazingira.
Aidha Makamu wa Rais ameongeza kwamba Tanzania itaendelea kufanya jitihada za ndani za kukabiliana na uharibifu wa mazingira pamoja na kutekeleza ahadi zake ilizotoa katika jumuiya za kimataifa za uhifadhi wa mazingira ikiwemo kukabiliana na taka za plastiki,taka ngumu,taka oevu pamoja na kulinda bionuai. Makamu wa Rais ameipongeza serikali ya Sweden kwa kuchukua ajenda ya mazingira kuwa kipaumbele katika nchi yao pamoja na kuongoza mkutano wa kimataifa wa mazingira unaotarajiwa kufanyika Juni mwaka 2022.