Featured Kitaifa

UKAGUZI WA DAWA NA BIDHAA ZA AFYA KIPIMO CHA WAGANGA WAKUU MIKOA

Written by mzalendoeditor

OR- TAMISEMI

Naibu Katibu Mkuu( Afya) Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Grace Magembe amesema kuanzia sasa ukaguzi wa bidhaa za afya itakuwa ni moja ya kiashiria cha ufanisi kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri.

Ameyasema hayo leo tarehe 3 Machi,2022 alipofanya ukaguzi wa ubora wa utowaji wa huduma za afya katika Halmashauri ya Gairo na Mvomero Mkoani Morogoro ulioambatana na ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma ya afya inayoendelea kutekelezwa.

Dkt. Grace amesema kuwa kutofanyika kwa ukaguzi wa dawa na bidhaa za afya kunaweza kuchangia upotevu na matumizi mabaya ya bidhaa za afya ikiwemo dawa, vitendanishi na vifaa tiba
Amesema kazi ya ukaguzi wa bidhaa za tiba sasa lazima ifanyike kwa ushirikiano kati ya Idara ya Afya na Wakuu wa Idara nyingine wakiwemo wakaguzi wa ndani.

Amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kwa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kufanya ukaguzi wa bidhaa za afya kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mvomero na kuwasilisha taarifa kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI ndani ya siku 7 kufuatia ukaguzi wa awali kuonyesha kuna bidhaa ambazo takwimu zake hazikuwa na uhalisia

Aidha, amemuelekeza Mkurugenzi huyo kuanza mara moja ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura(EMD) na kumtaka Mhandisi wa Halmashauri kutoa utaalam wa kiufundi wa namna bora ya kuweka mifereji ya kuondoa maji yanayotuama katika eneo hilo.

About the author

mzalendoeditor