Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Sayi Magessa akifungua kikao kazi cha Kikosi Kazi cha Taifa cha Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Tanzania kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Zainab Chaula jijini Dodoma. 

Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mtoto Sebastian Kitiku akieleza lengo kikao kazi cha Kikosi Kazi cha Taifa cha Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Tanzania kilichofanyika jijini Dodoma.  

Baadhi ya wajumbe wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Tanzania wakifuatilia mada mbalimbali katika kikao kazi kilichowakutanisha jijini Dodoma.

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM

**************************

Na WMJJWM- Dodoma

Wizara za Kisekta zimehimizwa kuhakikisha zinatenga Bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ili kuweza kutekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Watoto.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Sayi Magesa katika ufunguzi wa kikao cha kikosi kazi cha Taifa cha Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa niaba ya Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula. 

Magesa amesema kuwa ili kuhakikisha afua za utekelezaji wa Programu hiyo zinatekelezwa lazima Wizara zijumuishe afua hizo kwenye mpango wake wa Bajeti.

Ameongeza kuwa Programu hiyo imeandaliwa kwa ajili ya kutatua changamoto zilizokuwepo pamoja na kuharakisha upatikanaji wa matokeo chanya katika utoaji wa huduma za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa kuhusisha sekta zote zinazohusu afya, lishe, ujifunzaji wa Awali, Malezi yenye mwitikio, ulinzi na usalama wa Mtoto nchini.

“Katika hili la kutenga Bajeti niwatake pia wadau wa maendeleo muongeze uwekezaji katika kutekeleza afua za Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ili kuongeza kasi kwenye utekelezaji wa Programu hii.

Aidha Magesa amesema utekelezaji wa Programu hii umesaidia uratibu wa afua zilizopo katika upatikanaji wa taarifa na takwimu sahihi katika kuboeresha utoaji wa huduma za Malezi na Makuzi watoto.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Tanzania Mwajuma Rwebangira amewaasa wadau kuendelea kujitokeza kushirikiana na Serikali kuhakikisha Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto inatekelezeka na kuleta matokeo chanya katika jamii.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Bright Jamii Initiatives Godwin Mongi amesema kuwa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto imelenga hasa kuifikia jamii hasa wazazi, walezi na watoto katika kuhakikisha suala la malezi linakuwa ni la umuhimu ili liweze kusaidia kupata watoto watakaoleta mabadiliko na maendeleo katika jamii zao.

Akizungumza katika kikao hicho Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Kija Banka amesema Wizara hiyo kupitia Jeshi la Polisi nchini itahakikisha watoto wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili tangu wakiwa wadogo na kuwaasa wazazi kuchukua hatua za kuwalinda watoto wao dhidi ya vitendo vya ukatili kwa kutimiza jukumu la malezi.

Hivi karibuni Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ilizindua Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM).

Previous articleEWURA YATANGAZA BEI MPYA ZA MAFUTA
Next articleNGAIZA FOUNDATION WASIMAMA NA RAIS SAMIA KUPIGANIA ELIMU BORA KWA MTOTO WA KIKE.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here