Uncategorized

NAIBU WAZIRI SAGINI ATEMBELEA VITUO VYA POLISI NA MAKAZI YA ASKARI YALIYOLALAMIKIWA BUNGENI, ZANZIBAR.

Written by mzalendoeditor

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini akizungumza na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Mwantumu Mdau Haji pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Rashid Hadidi alipotembelea Kituo cha Polisi cha Makunduchi, ikiwa sehemu ya ziara yake Zanzibar.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini akizungumza na Maafisa wa Polisi na wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar, kwenye kikao cha pamoja kilichofanyika leo katika ukumbi wa Chuo cha Polisi Zanzibar baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili visiwani humo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini akikagua ujenzi wa Vituo vya Polisi vipya vya Kizimkazi Dimabani, Daraja C pamoja na Kituo cha Polisi Mkokotoni, Daraja A Kaskazini Unguja leo, ikiwa sehemu ya ziara yake visiwani Zanzibar.

………………………………………………………..

Na Mwandishi wetu, MoHA.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini ametembelea Ofisi za Makamanda wa Polisi wa Mkoa na Wilaya, Vituo vya Polisi na Makazi ya askari wa Jeshi la Polisi Zanzibar, vilivyolalamikiwa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Zanzibar, katika Bunge lililopita.
Naibu Waziri Sagini ametembelea maeneo hayo, ili kufahamu changamoto, mapungufu waliyonayo pamoja na kupata suluhisho ya changamoto hizo.

Vituo vya Polisi pamoja na Makazi ya Askari wa polisi Zanzibar yaliyolalamikiwa na kutembelewa na Naibu Waziri Sagini ni Kituo cha Polisi Uzi, Kituo cha Polisi Bet-Ras, Kituo cha Kidongo-Chekundu, Kituo cha Polisi Mwanakwerekwe, Kituo cha Polisi Chukwani, Kituo cha Polisi Mwembemadafu pamoja na Kituo cha Polisi na Makazi ya Polisi Makunduchi Zanzibar.

“Katika Bunge lililopita, lilikuwa na maswali mengi sana ya Wabunge wanaowakilisha Ubunge kutoka Zanzibar yalioashiria kwamba pana mambo yanahitaji kufuatiliwa na Wizara yetu hususan kwenye vituo vya polisi, makazi ya askari, ofisi za makamanda wa Polisi” Sagini alisema .

Naibu Waziri Sagini alisema hayo leo, Februari 28, 2022 wakati akizungumza na Maofisa wa Polisi pamoja na wa Idara ya Uhamiaji katika ukumbi wa Chuo cha Polisi Zanzibar, baada ya ziara yake ya siku mbili.
Hata hivyo Naibu Waziri Sagini amesema kuwa baada ya kupitia Vituo hivyo vya Polisi pamoja na makazi ya askari Wizara ya Mambo ya Ndani itajipanga pamoja na Jeshi la Polisi kuzifanyia kazi hatua kwa hatua changamoto hizo na kuboresha miundombinu hiyo.

“Vituo vyote vilivyolalamikiwa vitafanyiwa kazi, vituo vyote vilivyokuwa vimefungwa tayari vimerejeshwa kwenye kutoa huduma” alisema.

Naibu Waziri Sagini pia amelipongeza Jeshi la Polisi kwa ujenzi wa Vituo vipya vya Polisi vilivyojengwa Unguja Zanzibar.

Aidha akizungumza na Maofisa wa Polisi pamoja na wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Waziri amewataka Viongozi wa Polisi Kamsheni ya Zanzibar wasione ‘muhali’ huruma kuwawajibisha na kuwaadhibu askari wanaokiuka maadili ya kazi wa cheo chochote. Amesema Jeshi la Polisi lina wimbo wa maadili mzuri sana na ametaka kila askari kuyazingatia maneno ya wimbo huo katika utendaji wake wa kazi.

“ Nimekuja kuwakumbusha juu ya wajibu wenu. Polisi ndio chombo cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinachosimamia utekelezaji wa Sheria kwahiyo, Wizara inataka kuwakumbusha wajibu wenu kwa kuzingatia miiko ya maadili na Sheria inayosimamia Jeshi la Polisi”

Pia amelitaka Jeshi la Polisi Zanizbar kuendelea kufanya doria na kuimarisha utendaji kazi wao kwenye maeneo hatarishi ili watalii wazidi kuingia Zanzibar na kupelekea kukuza uchumi.

About the author

mzalendoeditor