Featured Kitaifa

WATU 26 KATI YA 100 WANA TATIZO LA UGONJWA WA SHINIKIZO LA JUU LA DAMU NCHINI

Written by mzalendoeditor

Amina Mollel mkazi wa Arusha ambaye anaishi na ugonjwa wasaratani ya kizazi na Virusi vya UKIMWI akieleza jinsi anavyoishi na magonjwa hayo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuyafahamu magonjwa yasiyoambukiza yaliyoandaliwa kwa wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua kikuu, madawa ya kulevya na magonjwa yasiyoambukiza, watu wanaoishi na magonjwa hayo na wahariri wa vyombo vya
habari. Washiriki 64 walihudhuria mafunzo hayo ya siku mbili yaliandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) yaliyofanyika katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam.

Prof. Beatus Kundi akielezea andiko la mkakati wa utetezi juu ya masuala ya lishe na kushughulisha mwili katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuyafahamu magonjwa yasiyoambukiza yaliyoandaliwa kwa wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua kikuu, madawa ya kulevya na magonjwa yasiyoambukiza, watu wanaoishi na magonjwa hayo na wahariri wa vyombo vya habari. Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyomalizika jana katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam yaliandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA).

Washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuyafahamu magonjwa yasiyoambukiza ambao ni wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua kikuu, madawa ya kulevya na magonjwa yasiyoambukiza, watu wanaoishi na magonjwa hayo na wahariri wa vyombo vya habari wakiwa katika makundi wakijadili sheria mbalimbali zitakazosaidia kutokomeza magonjwa hayo. Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyomalizika jana katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam yaliandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA).

………………..

Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

Utafiti wa viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza uliofanyika nchini mwaka 2012 unaonesha watu 26 kati ya 100 wanamatatizo ya magonjwa ya shinikizo la juu la damu na tisa kati ya 100 wanamatatizo ya kisukari.

Aidha hadi sasa  kuna visa vipya vya magonjwa ya saratani takribani elfu 40 kwa mwaka na ongezeko kubwa la magonjwa ya figo yanayohitaji usafishwaji wa damu na upandikizwaji wa figo.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Msaidizi Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya Dkt. James Kiologwe wakati akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuyafahamu magonjwa yasiyoambukiza yaliyoandaliwa kwa wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua kikuu, madawa ya kulevya na magojwa yasiyoambukiza, watu wanaoishi ya magonjwa hayo na na wahariri wa habari yaliyofanyika katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kiologwe alisema kuongezeka kwa wagonjwa wenye matatizo ya magonjwa  yasiyoambukiza kumeifanya Serikali kutumia fedha nyingi kuyatibu magonjwa hayo hivyo basi ni lazima kuwepo na uwekezaji mkubwa na wakutosha ili kuzuia watu wasipate magonjwa hayo, lakini wale wachache watakaopata magonjwa hayo  watambulike mapema kabla hawajapata madhara zaidi na hii itasaidia kukuza uchumi wa nchi wetu kwasababu jamii yenye afya bora hushiriki vizuri katika kukuza maendeleo ya nchi.

“Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua programu ya taifa ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza mwaka 2019 ili kuongeza chachu ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza nchini yanayoongezeka kwa kasi nasi tupo hapa kuendeleza gurudumu hilo ili kujenga jamii isiyo na magonjwa yasiyoambukiza”,.

“Kampeni ya kitaifa ya kubadilisha mtindo wa maisha italenga zaidi kutoa elimu kwasababu elimu ndio njia kubwa itakayoweza kuokoa maisha ya jamii yetu lakini pia kupata ushiriki mpana wa sekta mbalimbali katika kuzuia vichocheo  vinavyosababisha magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Dkt. Kiologwe.

Aidha Dkt. Kiologwe alisema katika mafunzo hayo wajumbe wamefanya  uchambuzi wa kisera kuhusiana na masuala ya lishe kwasababu suala la ulaji ni suala mtambuka ambalo linahitaji ushiriki wa sekta mbalimbali kuangalia namna vyakula vinavyopatikana na kuandaliwa kama vile vyakula vya sukari, vyakula vyenye chumvi, pombe na vimiminika vingine vinavyozalishwa na kutumika.

“Baada ya uchambuzi huo wa kisera wadau wanatarajia kutumia chambuzi na takwimu watakazopata kutengeneza kampeni ya kitaifa ya kubadilisha mtindo wa maisha kwa itakayosaidia kuondoa viashiria na changamoto mbalimbali zinazopeleka watu kupata magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Dkt. Kiologwe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Kisukari Tanzania (TDA) na mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) Prof. Andrew Swai alisema wadau mbalimbali walianza kufanya tafiti za magonjwa yasiyoambukiza ili kuona yameenea kwa kiasi gani tangu mwaka 1986 ambapo kwa wakati huo ilionekana watu kutoka maeneo ya vijijini ndio walikuwa na magonjwa yasiyoambukiza kwa wingi.

“Mwaka 1986 tafiti zilizofanyika katika mkoa wa Dar es Salaam zilionesha asilimia 3 ya watu walikutwa na ugonjwa wa kisukari, asilimia 5 walikutwa na Shinikizo la damu na mafuta kuzidi kwenye damu ilikua ni aslimia 5 lakini sasa kutokana na maendeleo na teknolojia asilimia ya magonjwa yasiyoambukiza yanazidi kukuwa kwa kasi hasa maeneo ya mijini”,

“Magonjwa yasiyoambukiza kwa kiwango kikubwa yamekuwa yakichochewa na vichocheo mtambuka kama vile mitindo isiyo bora ya maisha hasa ulaji usiofaa, kutokufanya mazoezi, unywaji wa vilevi, na matumizi ya sigara, ni wakati sasa jamii ibadilike magonjwa haya yasiwe tena vizuizi vya maendeleo katika familia zetu”, alisema Prof. Swai.

Amina Mollel mkazi wa Arusha ambaye anaishi na  saratani ya kizazi na Virusi vya UKIMWI alisema mfumo wa maisha aliokuwa akiuishi ulipelekea yeye kupata saratani ya shingo ya kizazi ugonjwa ambao jamii yake hawakuupokea vizuri hivyo kumfanya kuwa mnyonge katika jamii yake lakini baada ya kuhudhuria kliniki na kupata elimu sahihi amekuwa mtoa elimu ngazi ya jamii hivyo kufikisha elimu sahihi ya ugonjwa huo katika jamii inayomzunguka.

“Nilivyomaliza kliniki yangu ya kwanza katika Taasisi ya Saratani  Ocean Road na kurudi mtaani nilishangaa watu wengi ukiongelea saratani hawajui kama ndio kansa na ukiongelea kansa hawajui kama ndio saratani hivyo kugundua kuwa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza bado haipo katika ngazi za jamii”,.

“Nimefurahi leo kuona katika mkutano huu waandishi wa habari wamealikwa, wanapotoka hapa wakawe chachu ya kuilisha jamii elimu ya magonjwa yasiyoambukiza, yanasababishwa na nini, changamoto zake na nini kifanye ili jamii isipate magonjwa hayo kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wameokoa maisha ya watu wengi”, alisema Amina.

Naye George Kwayu ambaye ni mgonjwa wa kisukari kwa miaka 23 sasa alisema wagonjwa wa kisukari wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali ikiwemo upokeaji hasi wa tatizo la kisukari na jamii kuwa na mtazamo hasi juu ya ugonjwa huo hivyo kuwakatisha tamaa wagonjwa hao.

Kwayu alisema wagonjwa wa kisukari kama watafuata maelekezo wanayopewa na wataalam wa afya maisha yao yatarejea katika hali ya kawaida kwani wengi hupoteza maisha kwa kudharau ama kutokufuata maelekezo waliyopewa na wataalam wa afya na wengine hupoteza maisha kutokana na ugumu wa maisha hivyo kushindwa kumudu gharama za matibabu.

“Nimepitia changamoto nyingi tangu nikiwa mdogo baada ya kugundulika ninatatizo la kisukari nikiwa na umri wa miaka mitatu, shule nyingi zilikuwa zikinikataa kuwa naweza kuanguka na kufa wakati wowote hivyo kunipa wakati mgumu katika kutimiza ndoto zangu, lakini pia jamii imekuwa ikitunyooshea mkono kuwa sisi wagonjwa wa kisukari hatuwezi kupata watoto pasipo kuwa na elilmu juu ya ugonjwa huu wa kisukari”, alisema Kwayu.

Washiriki 64 walihudhuria mafunzo hayo ya  siku mbili yaliandaliwa na  Wizara ya Afya kupitia  Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania  (TANCDA)  yaliyofanyika katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam.

About the author

mzalendoeditor