Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ya jibu hoja zilizotolewa na taasisi ya Creative Industry Network Tanzania (CNIT) kwa kushirikiana na Twaweza na kusisitiza suala la ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha siyo la uanaharakati ni suala la kisheria.
Kauli hiyo imetolewa leo Februari 22, 2022 na Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Tanzania Doreen Anthony Sinare katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Akiendelea kuzungumza Afisa Mtendaji Mkuu huyo alieleza kuwa Kanuni ya usajili wa wanachama na kazi zao inataka wabunifu wa Hakimiliki, Asasi na Makundi yanayojihusisha Hakimiliki kujisajili COSOTA ili waweze kutambuliwa , hivyo taasisi ya CNIT wala Mkurugenzi Mtendaji wake Robert Mwampembwa pamoja na Twaweza hazitambuliki na COSOTA.
“Kwa mdau yoyote aliyekuwa na maswali, hoja au maoni kuhusu mgao wa mirabaha uliyofanyika hivi karibuni anakaribishwa ofisini kuuliza na siyo kuanza kufanya upotoshaji kwa kuandika au kuzungumza vitu visivyo vya kweli COSOTA inakemea vikali tabia hii,”alisema Doreen.
Pamoja na hayo Bi. Doreen alifafanua kuwa COSOTA haijakusanya mirabaha kutoka katika Redio Saba tu kama ilivyoelekezwa bali imekusanya kutoka vyanzo mbalimbali kama Baa, Hoteli, Kumbi za Sherehe, Kumbi za Starehe na vyombo vya habari kama Kebo, Redio na Televisheni.
Aidha, Mtendaji Mkuu huyo wa COSOTA amefafanua kuhusu hoja ya fedha zilizopokelewa kutoka taasisi ya Hakimiliki ya CAPASSO ya nchini Afrika ya Kusini, kiasi cha Milioni ishirini na moja kupelekwa katika mfuko wa Sanaa na Utamaduni nikutokana na fedha hizo kuwa na viwango vidogo kwa wanufaika ambapo mara baada ya kugawa wanufaika walikuwa akipata kiasi cha Tshs. 2,214 na hapo zilihitajika kukatwa 5%.
Hivyo COSOTA inatoa wito kwa wabunifu wote kuendelea kusajili kazi zao kwa ajili ya kuziwekea ulinzi, na inasisitiza kuwa mgao wa mirabaha unatokana na matumizi ya kazi kibiashara na siyo kwamba unaposajili tu kazi yako unakuwa unastahili kulipwa mrabaha.