Featured Kitaifa

BILIONI 9.3 ZATOLEWA NA SERIKALI UTEKELEZAJI WA ELIMU BILA ADA MKOANI KAGERA

Written by mzalendoeditor

Na. Angela Msimbira NGARA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amesema hadi kufikia Januari, 2022 shilingi bilioni 9.3 kwa ajili ya kuendeleza sera ya elimu bila Ada Mkoani Kagera

Ameyasema hayo leo tarehe 22 Februari, 2022 wakati alipohutubia wananchi kwenye maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Utumishi wa Kiaskofu Severine Niwemugizi wa Jimbo la Lulenge – Ngara Mkoani Kagera.

Waziri Bashungwa amesema Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya ukamilishaji wa madarasa ya shule za sekondari na msingi 167 na kuwezesha kujenga maabara 72 lengo ni kupunguza uhaba wa maabara mashuleni.

Sambamba na hilo Waziri Bashungwa amesema Mkoa wa Kagera kulikuwa na kata 11 ambazo hazikuwa na shule za Sekondari hivyo, Serikali imetoa shilingi bilioni 7.7 kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari kwenye kata ambazo hazikuwa na shule za Sekondari.

Waziri Bashungwa ameendelea kusema kwa Mkoa wa Kagera kiasi cha shilingi bilioni 15 . zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 116 ya shule za sekondari ambayo yamewezesha kupunguza msongamano mashuleni.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na taasisi za dini hasa katika suala la kuleta maendeleo kwa jamii na kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi.

Amesema kuwa Taasisi za dini zinashirikiana na Serikali katika maendeleo na kuwahudumia wananchi, hivyo kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI iliunda timu ya kuangalia maeneo ambayo yanashirikiana na Taasisi za dini katika kutoa huduma mbalimbali hususani huduma za afya na kuangalia namna ya kushirikiana katika utoaji wa huduma bora kwa jamii.

Aidha, amechukua nafasi hiyo kumpongea Askofu Niwemugizi kwa kufikisha Jubilei ya Miaka 25 ya uaskofu.

About the author

mzalendoeditor