Featured Kitaifa

NABII JOSHUA ASHINDA URAIS UMOJA WA MITUME NA MANABII TANZANIA

Written by mzalendoeditor

NA MWANDISHI WETU

KIONGOZI Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania,Dkt. Nabii Joshua Aram Mwantyala ametwaa asilimia 80 ya kura katika uchaguzi wa nafasi ya urais katika Umoja wa Manabii na Mitume nchini Tanzania (Unity of Apostles and Prophets Tanzania).

Ushindi huo umetokana na kura 179 alizopata huku akiwaacha mbali washindani wake akiwemo Mchungaji Ceasar Masisi aliyepata kura 42 na Mtume Joackim aliyepata kura nne kupitia uchaguzi uliofanyika katika Ukumbi wa Anatoglo uliopo Ilala, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Askofu Profesa Rejoice Ndalima alimtangaza rasmi Dkt.Nabii Joshua Aram Mwantyala kuwa Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii nchini Tanzania.

Aidha, mitume na manabii mbalimbali nchini walionesha imani kubwa juu ya Dkt. Nabii Joshua huku wakimpongeza na kuahidi kumpa ushirikiano mkubwa aweze kutekeleza jukumu lake la kuwaunganisha viongozi hao wa kiroho ili waweze kulihubiri neno la Mungu kwa ufanisi nchini.

Wakati huo huo akizungumza baada ya kutangazwa mshindi katika nafasi hiyo, Dkt. Nabii Joshua amesema kuwa, anakwenda kusimamia mambo makuu matatu ikiwemo kusimamia na kuhamasisha umoja kwa mitume na manabii.

“La kwanza, Bwana Yesu alitoa maelekezo siku chache kabla ya kuondoka kuhusu umoja, na matokeo ya umoja, tunaona kina Petro baada ya siku ile ya Pentekoste waliwainua viwete, kazi yangu itakuwa kuhakikisha ninasimamia na kuhamasisha umoja,kukesha na kuombea umoja wa mitume na manabii wa kanisa la Tanzania,”amesema Dkt.Nabiijoshua.

“Nina hakika katika umoja huo tutaenda mahali,tutasimama mahali aliposimama Petro alipomfuata Dorcas,”amesema.

Kiongozi huyo ambaye ni mzaliwa wa Mbeya akiwa amebatizwa kama Mpentekoste amesema ana zaidi ya miaka 20 katika wito akiwa ndiye kiongozi na mwanzilishi wa Huduma ya Haki Ministry makao makuu yakiwa mkoani Morogoro yenye matawi zaidi ya 200 nchini.

“Pili nitahakikisha umoja wetu unakuwa na faida kwa Taifa letu la Tanzania hasa katika kipindi hiki ambacho Taifa letu la Tanzania limempata Rais mwanamke, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Debora hakwenda peke yake, kwa hiyo sisi tutakwenda na Debora wetu Rais wetu Mheshimiwa Samia kumsaidia kazi

“La mwisho nitahakikisha ninasimamia mitume na manabii kuhakikisha tunarudi katika misingi ya wazee wetu. Kitabu cha Malaki, Biblia inasema nitageuza mioyo ya watoto wawaelekee baba zao. Nitahakikisha tunawaenzi wazee wetu wakiwemo Baraza la Wapentekoste kwa kazi kubwa waliyoifanya, kwa sababu sisi ni matunda ya kazi yao,”amesema Dkt.Nabiijoshua,

About the author

mzalendoeditor