Featured Kitaifa Uncategorized

‘TUMETENGA BILIONI MOJA KUENDELEZA WABUNIFU WATAKAOIBULIWA MAKISATU 2022’:WAZIRI MKENDA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda,akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 16,2022  kuhusu maadhimisho ya Wiki  ya Ubunifu na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu maarufu kama (MAKISATU) kwa mwaka 2022 ambapo kilele cha Mashindano hayo kufanyika Mei 15 hadi 20,2022 jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Juma Kipanga,akifafanua jambo kuhusu maadhimisho ya Wiki  ya Ubunifu na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu maarufu kama (MAKISATU) kwa mwaka 2022 kilele cha Mashindano hayo kufanyika Mei 15 hadi 20,2022 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Eliamani Sedoyeka,akizungumzia mikakati ya wizara katika kuhusu maadhimisho ya Wiki  ya Ubunifu na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu maarufu kama (MAKISATU) kwa mwaka 2022 kilele cha Mashindano hayo kufanyika Mei 15 hadi 20,2022 jijini Dodoma.

……………………………………………………………

Na.Alex Sonna,DODOMA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda,amesema kuwa Serikali imetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuwaendeleza wabunifu watakao tambuliwa kwa mwaka 2022 kupitia mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu MAKISATU.

Hayo ameyasema leo Februari 16,2022  jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Wiki  ya MAKISATU kwa mwaka 2022 ambapo amesema serikali imetenga kiasi hicho ili kuendeleza bunifu zitakazoibuliwa kupitia mashindano hayo kwa mwaka 2022.

“Wiki ya ubunifu ni sehemu ya mikakati ya serikali ya awamu ya sita ya kuongeza hamasa ya matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo za kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii” amesema Prof. Mkenda.

Akizungumzia wiki ya ubunifu inayoandaliwa kwa kushirikiana na program ya funguo ya shirika la UNDP amesema itafanyika katika mikoa 17 ambayo ni Dar es saalam, Dodoma, Mbeya, Arusha, Iringa, Mwanza, Zanzibar, Tanga, Kilimanjaro, Morogoro.

Mikoa mingine ni Njombe, Kagera, Mtwara, Kigoma, Mara na Ruvuma wakati kitaifa wiki ya ubunifu kwa mwaka 2022 itaadhimishwa kuanzia tarehe 15 hadi 20 Mai 2022 katika jiji la Dodoma itakayoenda sambamba na kilele cha MAKISATU.

Ameongeza kuwa “Usajili wa ubunifu kwa ajili ya Mashindano ulifikia mwisho tarehe 10, Februari, 2022, Lakini kutoka na uhitaji, Leo nichukue fursa hii kutangaza rasmi, kuongeza muda wa usajili wa Wabunifu hadi tarehe 28 Februari, 2022 hadi kufikia jana tarehe 15 Februari, tumesajili wabunifu zaidi ya 480 kwa ajili ya Mashindano. 

Aidha Prof Mkenda amesema mashindano ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, washiriki watatoka katika makundi saba ambayo ni Shule za Msingi Shule za Sekondari Vyuo vya Ufundi Stadi Vyuo vya Ufundi Vyuo Vikuu Taasisi za Utafiti na Maendeleo na Mfumo usio Rasmi.

“Usajili wa washiriki wa MAKISATU 2022 ulianza rasmi tangu tarehe 27 Desemba, 2021 na usajili huo unaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikishirikiana

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inayosajili wabunifu wa makundi ya Vyuo Vikuu na Taasisi za Utafiti na Maendeleo

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) inayosajili wabunifu wa makundi ya Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi na wale wa Mfumo usio rasmi Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi linalosajili wabunifu wa kundi la Vyuo vya Ufundi  na 

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa kushirikiana na Wizara inayosajili wabunifu wa makundi ya Shule za Msingi na Shule za Sekondari” amesema.

Vile vile Prof. Mkenda amebainisha kuwa katika kilele hicho kutakuwa na maonesho ya teknolojia na bunifu mbalimbali, bidhaa na huduma zinazotolewa na taasisi zitakazoshiriki zikiwemo taasisi za kitafiti na maendeleo, Vyuo Vikuu, kumbi za ubunifu, taasisi za kibiashara, wakala za Serikali, Wizara na Taasisi binafsi na pia katika kilele hicho kutakuwa na utoaji tuzo kwa wabunifu 21 walioshinda MAKISATU. 

Amesema wiki ya MAKISATU imelenga kuibua, kutambua na kuendeleza jitihada zinazofanywa na wabunifu wa Kitanzania na kuhamasisha matumizi ya Sayansi Teknolojia na ubunifu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amebainisha kuwa kupitia MAKISATU 2019, 2020 na 2021, Wizara imefanikiwa kuibua na kutambua wabunifu wachanga 1,785. Kupitia wabunifu hao bunifu 466 zilikidhi vigezo, zimetambuliwa na kuhakikiwa na kati ya hizo bunifu mahiri 200 tayari zinaendelezwa na Serikali ili kufikia hatua ya kubiasharishwa.

“Aidha napenda kutoa taarifa kuwa kati ya bunifu zinazoendelezwa na Serikali, 26 zimeshafikia hatua ya kubiasharishwa, wakati 95 ziko katika hatua ya Sampuli kifani (prototype) na nyingine katika hatua za awali za kuandaa sampuli kifani” amesema. 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omar Kipanga amesema kuwa katika wabunifu walioibuliwa wanalelewa katika vyuo vikuu na vyuo mbalimbali hapa nchini na kuendeleza na kulea bunifu hizo ili zifikie hatua ya kuingizwa sokoni.

About the author

mzalendoeditor