Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, atasherekea siku yake ya kuzaliwa kwa kuongoza zoezi maalum la upandaji miti litakalofanyika tarehe 27 Januari, 2026 katika maeneo ya Bungi Kilimo na Kizimkazi, Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa January 22,2026 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, zoezi hilo lina kaulimbiu “Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti” na ni sehemu ya kuendeleza ajenda ya Taifa ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa katika zoezi hilo kutafanyika upandaji miti, ulinzi wa vyanzo vya maji, uhifadhi wa uoto wa asili pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, zoezi hilo linaelezwa kuwa ni ishara ya uwajibikaji wa pamoja na linatoa fursa kwa kila mwananchi, kwa nafasi yake na mahali alipo, kushiriki katika kulinda na kuenzi mazingira kwa manufaa ya sasa na kizazi kijacho.
Mhe. Rais ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kujenga utamaduni wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa hiari, akisisitiza kuwa ulinzi wa mazingira ni msingi wa uhai, maendeleo na usalama wa Taifa.
