Mwenyekiti wa Tume huru ya kufanya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa 2025, Mhe. Mohammed Chande Othman, akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari, leo Disemba 1, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu (BOT), jijini Dar es Salaam.
….
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, Mhe. Mohammed Chande Othman, amesema Tume imeanza rasmi kazi yake na itafanya uchunguzi wa kina, wa wazi na wa kitaalam ili kutoa majibu yanayotarajiwa na Watanzania.
Akizungumza leo Disemba Mosic,2025 katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam, Jaji Mstaafu Chande amesema kuwa Tume hiyo imekabidhiwa majukumu makubwa sita ambayo ni msingi wa uchunguzi huo.
Amesema majukumu hayo ni pamoja na kuchunguza na kubaini chanzo halisi cha matukio ya vurugu wakati na baada ya uchaguzi, kuchunguza malengo ya waliohusika kupanga na kutekeleza machafuko, kubainisha mazingira ya matukio ikiwemo vifo, majeruhi na athari za kiuchumi na kijamii, pamoja na kuchambua hatua zilizochukuliwa na Serikali na taasisi zake kupambana na matukio hayo.
Majukumu mengine ni kupendekeza maeneo ya kuimarishwa ili kuongeza uwajibikaji wa viongozi na raia, kukuza utawala bora, haki za binadamu na kuimarisha mifumo ya majadiliano ya kitaifa ili kuepusha kurudia kwa matukio kama hayo, pamoja na kuchunguza masuala mengine yoyote yanayohusiana na kazi za Tume hiyo.
“Tume yetu iko huru kutafsiri hadidu za rejea na itafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchunguzi. Tutajikita hasa katika maeneo yaliyoathirika ili kubaini aina ya matukio, chanzo chake, athari zilizotokea na hatua zilizochukuliwa,” amesema Mhe.Chande
Jaji Mstaafu Chande amesema Tume itatumia njia mbalimbali kukusanya taarifa zikiwemo mapitio ya nyaraka, mahojiano ana kwa ana na kwa njia ya mtandao, dodoso la mtandaoni, barua pepe, barua za kawaida na ujumbe mfupi wa simu. Aidha, itafanya mijadala ya makundi na kushauriana na wataalam mbalimbali.
Aidha amewataka Watanzania kushirikiana na Tume kwa kutoa taarifa sahihi na za ukweli zitakazosaidia kufanikisha uchunguzi huo, akibainisha kuwa wananchi wanategemea Tume kufanya kazi kwa uwazi, ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara na kukusanya ushahidi wa moja kwa moja.
“Pamoja na uchungu tulioupitia kutokana na yaliyotokea, majibu ya mambo mengi tunayo sisi wenyewe. Tukisaidiana tutapata ukweli utakaotusaidia kuweka msingi wa mazungumzo ya maridhiano ya kitaifa,” amesema
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, wadau watakaoshirikishwa katika uchunguzi huo ni pamoja na waathirika wa machafuko, watuhumiwa, vyama vya siasa, asasi za kiraia, wasimamizi wa uchaguzi, Tume Huru ya Uchaguzi, viongozi wa dini, bodaboda, wamachinga, wafanyabiashara na wajasiriamali, sekta binafsi, watafiti, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na waandishi wa habari.
Tume hiyo inatarajiwa kutoa mapendekezo ya muda mfupi na mrefu yatakayosaidia kuimarisha mfumo wa kitaifa wa kuzuia na kudhibiti machafuko ya uchaguzi, huku ikilinda misingi ya amani, umoja na mshikamano wa Taifa.