Featured Kitaifa

WANANCHI WILAYA YA KAKONKO WATAKIWA KUACHANA NA MIKOPO UMIZA

Written by mzalendo

Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Evance Mallasa, akizungumza kuhusu changamoto ya mikopo umiza alipokutana na kuzungumza na Timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo inaendelea na zoezi la kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma. 

Na. Chedaiwe Msuya, WF, Kigoma.

Wananchi wa Wilaya ya Kankoko mkoani Kigoma, wametakiwa kuacha tabia ya kukopa fedha kwenye taasisi zisizo na leseni ya kutoa huduma za fedha ili kuepuka kuingia kwenye migogoro wakati wa kurejesha mikopo yao.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Kanali Evance Mallasa, alipokutana na Timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo inaendelea na zoezi la kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika Mkoa wa Kigoma. 

Kanali Mallasa alisema wananchi wengi wa Wilaya ya Kankoko wakiwemo watumishi wa umma wanakabiliwa na changamoto ya kuomba mikopo umiza maarufu kama kausha damu kwenye taasisi zisizo rasmi jambo linalosababisha kutapeliwa na kuingia kwenye wimbi la umasikini.

“Mikopo hii ya kaushadamu kwakweli imekuwa ikiwaumiza sana wananchi na watumishi wa Serikali kutokana na riba kubwa inayowekwa na wakopeshaji pasipo kufuata taratibu za mikopo jambo ambalo halina afya kwa ustawi wa wananchi wetu”, alisema Kanali Mallasa.

Alisema kuwa mikopo inayotolewa mtu akifuatilia hawezi kuona mikataba ambayo hutolewa kwa uwazi bali imejificha na kusababisha wananchi kutoa marejesho makubwa kutokana na riba kubwa, hali ambayo inawaumiza.

Kanali Mallasa alisema kuwa kama Mkuu wa Wilaya anawashauri watumishi na wananchi wote kwa ujumla kukopa kwenye taasisi rasmi kwa sababu kuna taratibu zinawekwa na zinafahamika kwa wananchi kwa uwazi.

Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha katika Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, amewataka wananchi kuwa na utamaduni mzuri wa masuala ya kutafuta na kutumia fedha.

“Nidhamu ya fedha ni pamoja na kile unachopata katika utendaji wa kazi katika biashara na utumishi kuendana na matumizi, watu wengi wamekuwa na matumizi mabaya ya fedha, anapata shilingi elfu kumi lakini matumizi yake ni 15,000,”alisema Bw. Kibakaya.

Alisema kuwa madhara ya kutumia fedha zaidi ya kipato ni kuingia kwenye mikopo ambayo sio salama, ni vema wananchi waweze kuwa na utaratibu wa kuandaa bajeti ili kile wanachopata kiwekewe utaratibu wa kutumia vizuri.

Naye mkazi wa kijiji cha Kabale Wilayani Kakonko, Bw. Ernest Mboko, alisema kutokana na elimu aliyopata imemfanya kuwa na uelewa wa kutafuta fedha, kuweka akiba na kufanya matumizi sahihi kulingana na mahitaji.

Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha inaendelea na utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi katika mikoa mbalimbali ili kuhakikisha wananchi na jamii inapata uelewa na kujifunza namna bora ya matumizi sahihi ya fedha na kujiepusha na matumzi yasiyo rasmi.

About the author

mzalendo