Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI MWANAIDI AOMBA BUNGE NA JAMII KUUNGA MKONO JITIHADA ZA SERIKALI MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI

Written by mzalendo

Na WMJJWM-Dodoma.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ameweka msisitizo kwa kuliomba Bunge na Jamii kwa ujumla kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili na mmomonyoko wa maadili nchini.

Naibu Waziri Mwanaidi ameyasema hayo wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati wa mawasilisho ya Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/25.

Naibu Waziri Mwanaidi amesema Serikali kupitia Wizara inaratibu na kusimamia afua za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ambazo ni Msingi muhimu katika ukuaji ili kujenga familia na Taifa lenye maadili mema.

Ameiomba Jamii kuzingatia suala la malezi kwa watoto wao kwa kuhakikisha wanapata muda wa kukaa na kuzungumza nao kuhusu masuala na changamoto mbalimbali zilizopo kwa wakati huu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Ameongeza kuwa, katika kuhakikisha mtoto analindwa na vitendo vya ukatili na mmomonyoko wa maadili, Wizara kwa kushirikiana na Wizara za kisekta inaendelea kufanya marekebisho ya Sheria mbalimbali zinazogusa suala la mtoto.

“Wizara yetu kwa kushirikiana na Wizara nyingine kama Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Katiba na Sheria itajadiliana na kuona namna ya kuwa na Sheria itayomlinda mtoto moja kwa moja na matumizi ya mitandao” amesisitiza Naibu Waziri Mwanaidi

Kuhusu Ustawi wa Wazee nchini Naibu Waziri Mwanaidi amesema Wizara ipo katika hatua ya mwisho ya kurekebisha Sera ya Wazee ili iweze kuendana na wakati uliopo na kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wazee nchini.

“Mambo muhimu yanayozingatiwa katika Sera hiyo ni kutoa elimu ya Wazee kujiandaa kustaafu, huduma za afya, msaada ya kisaikolojia, mazingira wezeshi, uwezeshaji wa wazee katika mabadiliko ya teknolojia yaliyopo” amesema Naibu Waziri Mwanaidi

Kwa upande wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Naibu Waziri Mwanaidi amesema Wizara inaendelea kuyaratibu na katika hilo imeanzisha ramani ya kidijitali itakayosaidia kutambua Mashirika hayo yalipo na yanafanya shughuli gani iliyozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Philip Isdory Mpango wakati wa Jukwaa la Mwaka la NGOs 2023.

“Hadi kufikia Aprili 2024 ramani imeweza kuyatambua Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 10,538 yalipo na kuonesha yanajishugulisha na Afua zipi ili kuhakikisha yanataribiwa vizuri kuondokana na Mashirika ambayo yanaweza kuhamasisha vitendo vya mmomonyoko wa maadili” amesisitiza Naibu Waziri Mwanaidi

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa mwaka wa fedha kiasi cha Billioni 67.9.

About the author

mzalendo