Featured Kitaifa

WAKUU WA SHULE, MADEREVA ZINGATIENI USALAMA WA WANAFUNZI KIPINDI CHA MVUA – MAJALIWA

Written by mzalendo

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa taarifa ya Serikali bungeni kuhusu changamoto za hali ya hewa nchini na kujibu maswali Bungeni jijini Dodoma, Aprili 25, 2024.

(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wamiliki wa shule na madereva wa mabasi yanayotoa huduma za usafiri kwa wanafunzi wajiridhishe kuhusu njia wanazopita ili kuhakikisha kunakuwepo na usalama wa wanafunzi wanaowabeba katika vyombo vya usafiri.

“Wazazi, Walezi na Jamii ya Watanzania kwa ujumla tushiriki kikamilifu katika kuhakikisha usalama wa wanafunzi wanapokwenda na kurudi Shuleni wakati wote hususan katika kipindi cha mvua.”

Kadhalika amesema kwa kuwa Serikali imetoa maelekezo ya kufunga shule zilizoathiriwa na mafuriko, halmashauri na wamiliki wa shule zisizo za Serikali waweke utaratibu wa kufidia muda wa vipindi ili kukamilisha kalenda ya muhula kama ilivyopangwa.

Ametoa wito huo leo (Alhamisi, Aprili 25, 2024) wakati akitoa taarifa ya serikali kuhusu changamoto  za hali ya hewa bungeni jijini Dodoma.

Pia, amezitaka Taasisi za Serikali ziendelee, kukabiliana na maafa kwa kushirikiana na wadau kutekeleza majukumu yaliyoanishwa katika Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El-Nino pamoja na mipango ya kisekta ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

“Kamati za Maafa za Wilaya na Mikoa ziendelee kuchukua hatua stahiki ikiwemo kutoa tahadhari kwa wananchi na kusaidia wananchi kwa wakati pindi maafa yanapojitokeza.”

Aidha, amewataka Wakuu wa mikoa na wilaya, maafisa tarafa, watendaji kata, mitaa na vijiji wasimamie ipasavyo usafi katika maeneo yao na kudhibiti utupaji taka ovyo unaosababisha kuziba kwa mitaro badala ya kusubiri usafi unaofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.

“Kwa kuwa uharibifu wa mazingira umekuwa na athari kubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi, viongozi wa ngazi zote washirikiane na wananchi kudhibiti uharibifu wa mazingira katika maeneo yao.”

Mheshimiwa Majaliwa pia amelitaka Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani liendelee kutoa tahadhari kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara wakati wa mvua;

“Kamati za Maafa katika ngazi za Vijiji, Wilaya na Mikoa zisimamie kikamilifu ugawaji wa misaada inayotolewa kwa waathirika wa mafuriko na kuhakikisha kuwa misaada inawafikia walengwa”.

Kadhalika amewataka Viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Vijiji wahamasishe na kuelimisha wananchi wanaoishi mabondeni kuhamia maeneo salama ili kuepusha maafa wakati wa mafuriko na kuhakikisha wanatenga maeneo salama yatakayotumika na wananchi watakaohamia kutoka mabondeni.

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amesema kutokana na maafa yaliyotokea nchini, Serikali kupitia Kamati za Usimamizi wa Maafa na wadau imechukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kuzuia, kukabiliana na kurejesha hali.

“Hatua hizo zinajumuisha utoaji wa elimu kwa jamii ya kujikinga na kuchukua tahadhari, kukabiliana na maafa na kurejesha miundombinu iliyoharibika. Aidha, Serikali imetoa misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula, vifaa vya ujenzi, vifaa vya malazi na vifaa vya usafi.”

Amesema, hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa na misaada kutoka Serikalini na wadau kama vile uokoaji, vyakula, mahema, madawa, marekebisho ya miundombinu ya utoaji huduma imeendelea kutolewa.

“Serikali imejipanga kikamilifu na inaendelea kuchukua hatua stahiki ili kuzuia na kupunguza makali ya majanga sambamba na kurejesha hali katika maeneo mbalimbali yaliyoathirika.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa nchini ikiwemo kufunga miundombinu ya kisasa ya hali hewa, mafunzo kwa watumishi kwa kuzingatia vigezo vya kitaifa na kimataifa, na kuweka mifumo wezeshi ya usambazaji wa taarifa ya hali ya hewa pamoja na kuimarisha mifumo ya uhakiki wa ubora wa huduma.

Amesema uwekezaji wa miundombinu uliofanyika unajumuisha ununuzi wa Rada za Hali ya hewa ambapo Rada mbili zinakamilishwa kufungwa katika mikoa ya Kigoma na Mbeya. Vilevile, Rada nyingine mbili zinatarajiwa kufungwa Mikoa ya Dodoma na Kilimanjaro ifikapo mwishoni mwa mwaka 2024.

“Nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika sekta ya hali ya hewa na kuijengea uwezo nchi yetu na kuifanya kuwa kinara Afrika na nje ya Afrika katika masuala ya utabiri wa hali ya hewa.”

About the author

mzalendo