Featured Kitaifa

WAZIRI MKUU AONGOZA MATEMBEZI YA AMANI

Written by mzalendo

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongoza Matembezi ya Amani, Maridhiano na Mama Samia Suluhu Hassan, kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam, Disemba 2, 2023. Kulia kwake ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Mkuu wa wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Taifa  wa  Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Sheikh Alhad  Salum.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki katika mazoezi ya viungo baada ya kuongoza Matembezi ya Amani, Maridhiano na Mama Samia Suluhu Hassan, kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam, Disemba 2, 2023. Kulia kwake ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Mkuu wa wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Maridhiano na Aman Tanzania, Sheikh Alhad Salum.

Waziri Mkuu, Kiassim Majaliwa akizungumza baada ya kuongoza   Matembezi ya Amani, Maridhiano na Mama Samia Suluhu Hassan, kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha Tuzo ya heshima aliyopewa   baada ya kuongoza   Matembezi ya Amani, Maridhiano na Mama Samia Suluhu Hassan, kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam, Disemba 2, 2023. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Mkuu wa wilaya ya Ilala  Edward Mpogolo na wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Sheikh Alhad Salum. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

…..

*Ampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha demokrasia

*Ahimiza wanaume wakapime VVU, wasitegemee matokeo ya wenza wao

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza matembezi ya amani, maridhiano na Rais Samia Suluhu Hassan na kuwataka viongozi wa dini waendelee kusisitiza amani miongoni mwa waumini wao.

“Viongozi wa madhehebu ya dini endeleeni kuwahimiza waumini wenu kulinda amani ya nchi yetu. Wafahamisheni waumini athari za kutozingatia thamani ya amani tuliyonayo huku mkisisitiza wajibu wa kila mmoja kuhakikisha amani inadumishwa hapa nchini,” amesema.

Ametoa wito huo leo (Jumamosi, Desemba 2, 2023) wakati akizungumza na washiriki na wadau mbalimbali kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, mara baada ya kushiriki matembezi hayo kwa km. 5 ambayo yameratibiwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT). 

Pia amewataka viongozi wa dini, washirikiane na Serikali katika kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi na gesi asilia ili kuinusuru nchi na athari za mabadiliko ya tabianchi.  

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini wawaeleze waumini wao kwamba licha ya mafanikio ambayo Serikali imeyapata kwenye mapambano dhidi ya VVU, wanapaswa watambue kuwa UKIMWI bado upo. 

“UKIMWI bado upo, ninawaomba suala hili lipewe kipaumbele wakati wa mahubiri, hotuba na mihadhara. Endeleeni kuwakumbusha waumini kuhusu umuhimu wa kubadili tabia hususan zile zinazochangia maambukizi.”

“Jana ilikuwa ni maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani. Kwenye tathmini yetu, malengo ya 95-95-95 yamefanikiwa kwa maana ya 95 ya kwanza imeongezeka kwa sababu watu wengi wamejitokeza kupima. Hii inahamasisha upimaji na watu wanaojitokeza ni wengi lakini wanaopima sana ni wanawake. Wanaume hamuendi kupima.” 

“Wanaume jitokezeni mkapime, msitegemee matokeo ya wake zenu. Mimi ndiye Balozi wa kuhamasisha wanaume kupima virusi vya UKIMWI, kwa hiyo msiniaibishe. Kuanzia leo, nendeni kwenye vituo vyetu mkapime VVU.”

Kuhusu 95 ya pili, Waziri Mkuu amesema hii imefanikiwa kwani waliopima na kugundulika wanatumia dawa kama inavyoshauriwa na 95 ya tatu imefanikiwa kwani wanaotumia dawa, kwa asilimia kubwa wamefanikiwa kufubaza virusi hivyo.

Amewataka viongozi hao wawaangalie zaidi vijana kwani ni kundi lililo kwenye hatari zaidi. “Kwa kuwa kundi la vijana liko katika hatari zaidi ya kupata maambukizi, ninawasihi sana imarisheni huduma za unasihi na malezi yenye mlengo wa kustahimili mabadiliko yanayotokana na utandawazi. Ninayo imani kuwa, kwa nafasi zenu ndani ya jamii, vijana watawasikia, watawatii na kubadilika.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuleta mtangamano na kukuza demokrasia. Kaulimbiu ya matembezi hayo ni: “Dumisha Amani, Maridhiano, Upendo na Udugu wa Kibinadamu.”

“Kipekee ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kunakuwepo na mtangamano wa kisiasa nchini unaojumuisha siasa safi, za kiustaarabu na zinazoheshimu mawazo ya kila mmoja wetu. Kutokana na maono na jitihada zake, hali ya siasa nchini ni tulivu na vyama vya siasa vinaendelea kutekeleza majukumu yao ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali nchini.”

Mapema, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Askofu Israel ole Gabriel Maasa alisema jumuiya hiyo ina matawi kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na kwenye wilaya zake. 

Akielezea mambo waliyofanikiwa kuyafanya hadi sasa, Askofu Maasa alisema: “Tumeongoza zoezi la uchangiaji damu katika baadhi ya hospitali nchini, tumefanya zoezi la upandaji miti, tumeshirikiana na Serikali kupinga unyanyasaji kwa watoto na wanawake, tumepinga ukatili dhidi ya wanaume na kuongoza mafunzo ya uraia kwa wananchi ili waipende na kuijali nchi yao.”

Akitoa salamu kwa niaba ya Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Ally Khamisi Ngeruko alisema: “Mufti na Sheikh Mkuu Dkt. Abubakar Zubeir bin Ally anasema Tanzania imejaa amani lakini Watanzania wanajipangaje kutumia fursa mbalimbali kwa kutumia amani tuliyonayo.”

About the author

mzalendo