Featured Kitaifa

DKT. BITEKO AIAGIZA TPDC KUANDAA MPANGO WA MUDA MREFU WA UPATIKANAJI GESI NCHINI

Written by mzalendo

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko akizungumza wakati wa kikao chake na Bodi na Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kilichofanyika jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mussa Makame akizungumza wakati wa kikao cha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko na Bodi pamoja na Menejimenti ya Shirika hilo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Balozi Ombeni Sefue akizungumza wakati wa kikao cha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko na Bodi pamoja na Menejimenti ya Shirika hilo.

Bodi na Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), wakimsikiliza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko (hayupo pichani) wakati wa kikao chake na watendaji hao.

…………

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza Bodi na Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuja na mpango wa muda mrefu utakaoonesha jinsi nchi itakavyoweza kuongeza kiasi cha gesi asilia ili muda wote kuwe na hazina ya kutosha ya nishati hiyo inayotumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuzalisha umeme, viwandani, majumbani na katika magari.

Dkt. Biteko ameyasema hayo tarehe 21 Novemba, 2023 wakati wa kikao chake na Bodi na Menejimenti ya TPDC ambacho kililenga kufahamiana, kubadilishana mawazo juu ya utendaji kazi na Mhe. Dkt. Doto Biteko kuelekeza matarajio ambayo nchi inayahitaji kutoka TPDC.

“TPDC tujiulize, Je uwezo wetu wa kuzalisha Gesi Asilia unaweza kujibu mahitaji yetu  ya Gesi ? tujiulize hili na tuchukue hatua. Tutambue kuwa mahitaji ya Gesi Asilia ni makubwa kwa sasa kwani dunia inahama kutoka matumizi ya mafuta na kwenda kwenye Gesi Asilia hivyo lazima tujipange, na pia tukumbuke tumesaini makubaliano ya kusafirisha
nishati hii kwenda Uganda, Zambia na Kenya hivyo lazima tuwe na Gesi ya kutosha.” Amesisitiza Dkt. Biteko

Dkt. Biteko pia amewataka TPDC kutokuwa na urasimu katika uchukuaji wa maamuzi mbalimbali ikiwemo kwenye shughuli za utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia ili kutorudisha nyuma sekta hiyo nchini.

Kuhusu maelekezo aliyoyatoa wakati wa ziara yake, katika Kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi na Kijiji cha Madimba na Msimbati mkoani Mtwara, Dkt. Biteko amesisitiza kuwa, maisha ya wananchi katika maeneo hayo ambayo kuna visima na mitambo ya Gesi Asilia lazima yabadilike na wapewe huduma bora ikiwemo maji, umeme, afya na usafiri.

“Nashukuru mmeanza kufanyia kazi maagizo niliyoyatoa kwa haraka, ikiwemo ya kuweka taa za barabarani Kijiji cha Msimbati, kupeleka umeme wa uhakika Madimba na Msimbati unaotoka kwenye mitambo ya Gesi Asilia, kupeleka kivuko kisiwa cha Songosongo na malipo ya mafao kwa wastaafu wa Knight Support ambao walikuwa wakilinda mitambo na visima vya Gesi Asilia Songosongo ambao hawakulipwa muda mrefu, watu hawa wanahitaji huduma bora.” Amesema Dkt. Biteko

Katika Hatua nyingine, Dkt. Biteko ameiagiza TPDC kupita kwenye Halmashauri zote nchini zinazopokea ushuru wa huduma kutokana na shughuli za Mafuta na Gesi Asilia kufanyika kwenye Halmashauri hizo ili TDPC ijihakikishie kwamba, fedha hizo zinaenda pia kwenye vijiji/maeneo ambayo shughuli za uzalishaji wa Gesi Asilia zinafanyika.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame alimweleza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuwa, TPDC inaandaa Mpango Mkakati wa Shirika (Corporate Strategic Plan) ambao utaweka mikakati ya Shirika kwa kipindi cha miaka 10 na zaidi ili kuwezesha upatikanaji wa Gesi Asilia ya kutosha kwa matumizi ya ndani na kuwekeza zaidi katika mnyororo wa thamani wa Mafuta na Gesi ili kukuza matumizi ya Gesi Asilia na hivyo
kuchochea biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

 Aidha alieleza mipango ya utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda kuja Tanzania, Mradi wa Gesi ya Kusindika (LNG) ambapo majadiliano yamekamilika na mikataba ipo kwenye hatua za kuidhinishwa, utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia katika Kisiwa cha Songosongo Magharibi unaotarajiwa kuanza Septemba 2025 na utafutaji mafuta kitalu cha Eyasi Wembere ambapo tafiti zinaendelea.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue amemshukuru Naibu Waziri Mkuu kwa maelekezo yake ambayo yamewapa hamasa ya kufanya kazi na wameahidi kwamba wataenda mbali kiutendaji na watatoa ushirikiano kwa Naibu Waziri Mkuu ili kusukuma mbali zaidi Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia nchini.

About the author

mzalendo