Featured Kitaifa

WAKUU WA VYUO, WARATIBU DAWATI LA JINSIA 612 KUPIGWA MSASA KUPAMBANA NA VITENDO VYA UKATILI VYUONI.

Written by mzalendo

Na WMJJWM Iringa

Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imesema imejipanga kutoa elimu kwa Wakuu wa Vyuo na Waratibu wa Dawati la Jinsia kutoka Vyuo Vikuu na Kati 612 ili kupambana na vitendo vya ukatili katika maeneo hayo.

Hayo yamebainika wakati wa kufunga mafunzo kwa Wakuu wa Vyuo na Waratibu wa Madawati ya Jinsia yaliyofanyika kwa siku mbili Oktoba 31 hadi Novemba 01, 2023 mkoani Iringa.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara hiyo Rennie Gondwe amesema katika mafunzo hayo ya siku mbili jumla Wakuu wa vyuo 21 na Waratibu 21 wamepatiwa mafunzo hayo, huku mpaka sasa jumla ya Vyuo 291 vikiwa vimepatiwa mafunzo hayo.

Aidha Rennie amesisitiza waratibu wa Dawati la Jinsia kutoka kwenye Taasisi hizo kufanya kazi kwa weledi ili kutokomeza vitendo vya ukatili vyuoni na katika jamii inayozunguka Taasisi hizo.

“Niwaombe waratibu wa Dawati la Jinsia mkafanye kazi kwa weledi na kuyafanyia kazi matukio ya ukatili kwa mujibu wa Kanuni na Taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha hakuna ukatili vyuoni na katika Jamii ” amesema bi Gondwe

Pia Bi Gondwe amesema, Dawati la Jinsia katika Vyuo vya elimu ya juu na ya kati lina wajibu wa kusimamia haki na kuendelea kutoa elimu juu ya athari za ukatili wa kijinsia kwa watumishi, wanafunzi na jamii kwa ujumla kwani kwa kufanya hivyo italeta chachu ya kutokomeza vitendo hivyo.

Amesisitiza waratibu hao kuhakikisha madawati hayo yanafikika kiurahisi kwa kuweka mfumo mzuri wa mawasiliano na utoaji wa Taarifa za ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake Mwezeshaji kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi Dkt Cyril Komba ametoa wito kwa Waratibu hao kutumia mafunzo hayo kwa kufuata mwongozo wa uendeshaji wa Dawati hilo ili kuhakikisha Jamii ndani na nje ya Taasisi hizo inapata huduma hiyo ili kupambana na vitendo vya ukatili vinavyoendelea kushamiri.

Naye Mwezashaji kutoka Ofisi ya Rais Utumishi Stariko Meshack amesema kwao kama wawezeshaji kikubwa wanategemea kuona kunakuwa na matokeo chanya ambayo ni kuona ukatili unatokomezwa kabisa, kwani kwa muda mrefu hakukuwa na mwongozo hivyo matukio mengi yalikosa sehemu ya kuyaripoti.

About the author

mzalendo