Featured Kitaifa

WAJASIRIAMALI MILIONI 8.6 WANUFAIKA NA MIKOPO YENYE THAMANI YA SH.TRILIONI 6.1

Written by mzalendoeditor

 

Katibu Mtendaji wa Baraza laTaifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi.Beng’i Issa,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Agosti 14,2023 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya masuala ya uwezeshaji Tanzania na vipaumbele kwa mwaka 2023/24.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya habari-MAELEZO Bw.Gerson Msigwa,akizungumza mara baada ya Katibu Mtendaji wa Baraza laTaifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi.Beng’i Issa,kutoa taarifa  kuhusu mafanikio ya masuala ya uwezeshaji Tanzania na vipaumbele kwa mwaka 2023/24.

Na.Alex Sonna-DODOMA

WAJASIRIAMALI milioni 8.6 wamenufaika na mikopo yenye thamani ya Sh.Trilioni 6.1 kupitia mifuko inayoratibiwa na Baraza laTaifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa mwaka 2022/23.

Hayo yamesemwa leo Agosti 14,2023 jijini Dodoma na Katibu Mtendaji wa Baraza laTaifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi.Beng’i Issa,wakati akizungumzana waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya masuala ya uwezeshaji Tanzania na vipaumbele kwa mwaka 2023/24.

Amesema kuwa  baraza linaratibu mifuko 72 ambayo ipo inayotoa mikopo ya moja kwa moja, dhamana, ruzuku pamoja na programu za uwezeshaji.

“Hadi Machi, 2023, hii imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya Sh.Trilioni 6.1 kwa wajasiriamali 8,650,257 wakiwamo wanawake 4,747,321 na wanaume 3,902,936,”amesema Bi.Beng’i

Hata hivyo amesema kuwa  mifuko na programu hizo zimetengeneza ajira 17,603,271 ambapo ajira kwa wanawake zilikuwa 9,248,916 (52.5%) na ajira kwa wanaume ni 8,354,355 (47.5%).

Aidha,amesema hadi kufikia Juni 2023 ajira 145,245 zimezalishwa kwa watanzania kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji (Local Content).

 Bi.Beng’i amesema  baraza linaratibu masuala ya ajira hiyo katika sekta za kipaumbele kama uziduaji (mafuta na gesi), kilimo, ujenzi, viwanda, utalii na sekta mtambuka.

“Hadi kufikia mwezi Juni 2023, jumla ya ajira 145,245 zimezalishwa kwa watanzania kupitia miradi hii ambapo wanawake 29,049 (20%) wamenufaika na wanaume 116,196 (80%) wamenufaika,” amesema Bi.Beng’i

Aidha amesema kuwa  kampuni za kitanzania zaid ya 1,700 zimenufaika kwa kupata kazi mbalimbali katika miradi hiyo.

Akizungumzia kuhusu Mpango wa Kuendeleza Viwanda Vidogo na vya Kati (SANVN Viwanda Scheme) unaolenga kutoa fursa kwa watanzania kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza Viwanda hususan vilivyochakata mazao ya kilimo na Mifugo, amesema hadi kufikia Juni 2023 Mpango huo umewezesha mikopo ya Sh. Bilioni 3.83 kwa miradi 65.

Hata hivyo amesema  miradi hiyo ilifanyika katika mikoa 13 ambayo ni Mwanza, Arusha Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya, Geita, Dodoma, Shinyanga, Iringa, Njombe, Singida, Pwani na Rukwa.

Pia amesema kuwa  hadi Machi, 2023 vituo vya uwezeshaji 18 vimeanzishwa katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Singida, Rukwa, Kigoma na Dodoma.

 Bi.Beng’i amesema kuwa vituo viwil kweye Morogoro na Pwani viko kwenye hatua za kuongeza huduma wezeshi na kuweza kuwa vituo vya uwezeshaji kamili.

“Vituo hivi vimeweza kutoa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 9.4 kwa wajasiriamali 4,017. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2022/23, Serikali ilitenga fedha za kuweza

kukarabati vituo katika Halmashauri tatu ambapo Nyang’wale imepewa Sh. Milioni 247, Mlele Sh. Milioni 69,8 na Mbinga Sh. Milioni 123.4.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya habari-MAELEZO Bw.Gerson Msigwa amewataka watanzania kujiepusha na mikopo inayoumiza na utapeli unaofanyika mitandaoni kuhusiana na mikopo hiyo.

”Watanzania nawaomba mjiepushe na mikopo umiza inayofanyika mitandao watu wanatumia utapeli kwa kutumia majina ya watu hali ambayo inasababisha watu kujikuta wanaingia kwenye mikopo ya kutepeliwa hivyo fateni taratibu za mikopo kupitia baraza hili”amesema Msigwa

About the author

mzalendoeditor