Featured Kitaifa

CFAO MOTORS YATAMBULISHA SUZUKI GRAND VITARA SEMI HYBRID INAYOTUMIA MAFUTA NA UMEME

Written by mzalendoeditor
Kampuni ya CFAO Motors Tanzania imezindua toleo jipya la gari aina ya Suzuki Grand Vitara Semi Hybrid 2023 ambayo injini yake inatumia mseto wa nguvu ya mafuta na umeme. Gari hilo limezinduliwa kwa mara ya kwanza katika soko la Tanzania na Afrika. 

 
Suzuki Grand Vitara 2023 inatazamiwa kuleta mapinduzi katika sekta ya magari hasa kwa kuzingatia kwamba imeundwa kwa teknolijia ya kisasa, ufanisi na ubora wa kiwango cha juu.  
 
Kampuni hiyo ambao ni wasambazaji wakuu wa magari barani Afrika, wamelenga kuwapa wateja wake magari ya kisasa na ya kibunifu zaidi katika soko. Suzuki Grand Vitara 2023 imeundwa ikiwa na muundo na muonekano mzuri, ufanisi katika uendeshaji na ufanisi katika matumizi ya mafuta. Gari hiyo ambayo ina injini ya mseto wa mafuta na umeme inafanya uzalishaji mdogo wa hewa ya kaboni na kuifanya kuwa gari rafiki katika utunzaji wa mazingira. 
 
Akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanyika Machi 24, 2023 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa CFAO Motors Tanzania, Francois Bompart alisema gari hiyo yenye uwezo wa kubeba watu watano inatarajiwa kuleta mapinduzi kwa watumiaji pamoja na sekta ya magari kwa ujumla. 
 
 
“CFAO Motors tumejitolea kuwapa wateja wetu magari ya kisasa na ya kibunifu zaidi. Tunayofuraha kutambulisha Suzuki Grand Vitara, gari ambayo injini yake inatumia mseto wa mafuta na umeme, gari hii imeundwa kuwa na ufanisi katika utendaji na pia katika matumizi ya mafuta,” alisema Bompart.
 
Mbali na ufanisi na muundo wa kuvutia nje na ndani ya gari, Suzuki Grand Vitara Semi Hybrid imesheheni sifa mbalimbali za kipekee kama vile mfumo wa skrini ya kugusa wa inchi tisa, uwezo wa kuunganisha smartphone, kuunganisha Bluetooth, kamera ya nyuma, udhibiti wa hali ya hewa kiotomatiki na zaidi. Gari hilo pia lina uwezo na sifa za kiwango cha juu za usalama kama vile breki za kuzuia kufuli, udhibiti wa uthabiti wa kielektroniki, usaidizi wa kuanza mlimani, na msururu wa mifuko ya hewa ili kuhakikisha usalama wa wakaaji wake.
 
Katika hafla ya uzinduzi, mhudhuriaji mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina alisisitiza kwamba gari jipya lililozinduliwa ni gari la kipekee kwa Watanzania wanaotaka kuendesha gari za kisasa na zinazoendana na teknolojia za kisasa.  
 
“Bila shaka, ubunifu na teknolojia iliyotumika kuunda gari hii ya Suzuki Grand Vitara Hybrid itawavutia watu wengi kujaribu magari ya kisasa. Nimesikiliza na kusoma mtandaoni sifa za gari hii na leo nimelijaribu hapa wakati wa uzinduzi, nimejiridhisha kwamba gari hii ni la kisasa”, alisema.
 
Suzuki Grand Vitara Semi Hybrid linapatikana katika duka la magari la CFAO Motors Tanzania jijini Dar es Salaam. 
 
Kwa habari zaidi kuhusu Suzuki Grand Vitara na sifa zake, tembelea tovuti ya Suzuki Tanzania – https://www.suzuki-tanzania.com/
 

About the author

mzalendoeditor