Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI SAGINI AWATAKA WASIMAMIZI WA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI KUWACHUKULIA HATUA WASIOFUATA SHERIA.

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Jumanne Sagini akizungumza na Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya zote nchini katika Kikao Kazi cha Kutathmini Utendaji kazi, Mafanikio na Changamoto wanazokutana nazo kilichofanyika katika ukumbi wa Jeshi la Polisi, jijini Dodoma leo, Agosti 11, 2022.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Camillus Wambura akizungumza kwenye kikao kazi cha Kufanya Tathmini Utendaji kazi, Mafanikio na Changamoto wanazokutana nazo Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya zote nchini kilichofanyika katika ukumbi wa Jeshi la Polisi, jijini Dodoma leo, Agosti 11, 2022.

Baadhi ya Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya zote nchini wakiwa katika Kikao Kazi cha Kutathmini Utendaji kazi, Mafanikio na Changamoto wanazokutana nazo kilichofanyika katika ukumbi wa Jeshi la Polisi, jijini Dodoma leo, Agosti 11, 2022.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Jumanne Sagini akiteta jambo na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Camillus Wambura kwenye kikao kazi cha Kutathmini Utendaji kazi, Mafanikio na Changamoto wanazokutana nazo Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya zote nchini,leo.

…………………………………………………….

Na Mwandishi wetu,

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini amewataka Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya (RTOs na DTOs) nchini kuendelea kuwachukulia hatua kali madereva sambamba na watumiaji wengine wa vyombo vya moto wasiotaka kufuata Sheria, Kanuni na Alama za Usalama Barabarani ambao wamekuwa chanzo cha kusababisha ajali zinazoendelea kujitokeza.

Akizunguma na Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya nchini, Naibu Waziri Sagini amewataka kuleta mabadiliko makubwa katika usimamizi wa Sheria za usalama barabarani na kuhakikisha mikoa yote inashirikiana kiutendaji ili kuwadhibiti madereva sugu na kuwachukulia hatua stahiki za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamani au kuwafungia leseni zao.

‘‘Wizara chini ya Mhandisi Hamad Masauni (MB) inapenda kuona   wasimamizi wa sheria za usalama barabarani wakidhibiti changamoto za barabarani na kuhakikisha barabara za Tanzania ni salama, kubadilishana uzoefu na kuhakikisha mikoa yote inashirikiana kiutendaji ili kuwadhibiti madereva sugu wanaovunja sheria’’ alisema.

Naibu Waziri Sagini aliyasema hayo 11 Agosti 2022 jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha kufanya tathmini ya utendaji kazi, mafanikio na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakati wanapotekeleza jukumu la kusimamia sheria za usalama barabarani.

Kikao kazi hicho cha siku tatu kinatarajia kutoka na mikakati ya kupunguza ajali za barabarani, kuondoa malalamiko kutoka kwa watumiaji wa barabara kwa kuwatendea haki kwa mujibu wa Sheria na kuwa na mpango kazi wenye tija katika kusimamia askari na Sheria za Usalama barabarani.

Akitoa pole kwa ndugu na jamaa wote ambao wamepoteza wapendwa pamoja na majeruhi waliotokana na ajali mbalimbali za barabarani, Naibu Waziri Sagini amewasihi watumiaji wote wa barabara hususani madereva, abiria, wapanda pikipiki watembea kwa miguu, wapanda baiskeli, wasukuma mikokoteni n.k kuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani, kuhakikisha watoto wadogo hawatembei barabarani peke yao, sambamba na kuacha kushabikia mwendokasi kwa Madereva na kuwaomba wananchi kusaidia kutoa taarifa za watakao kiuka Sheria za Usalama Barabarani ili wachukuliwe hatua.

“Napenda kuchukua nafasi hii kutoa pole kwa ndugu na jamaa wote ambao wamepoteza wapendwa wao kutokana na ajali mbalimbali za barabarani, nawasihi watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani” alisema

Aidha, Naibu Waziri Sagini amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Camillus Wambura kuchukua hatua stahiki kwa watendaji wasiowajibika ipasavyo na kusababisha  lawama zielekezwe kwa Jeshi zima la Polisi.

“IGP na Makamishna wako msione muhali kuwachukulia hatua stahiki wote wasiowajibika ipasavyo, lawama zitaelekezwa kwenu bila shaka hata matokeo ya lawama hizo yatawahusu” alisema.

About the author

mzalendoeditor