Featured Makala

RAIS SAMIA MWANASIASA,MWANADIPLOMASIA NA MLEZI WA JAMII

Written by mzalendoeditor

Na Hafidh Kido
KIONGOZI yeyote anayeshika madaraka ya nchi anatazamiwa kuwa kila kitu, jamii inategemea mambo yote wafanywe kutoka serikali kuu ambayo kiongozi wake ni rais wa nchi, kwengine ni Mfalme au Malkia.
Rais Samia Suluhu Hassan, wakati akiingia madarakani alisimamia jambo moja; alitaka kuwa mfariji mkuu wa Watanzania walioondokewa na kiongozi wao – Hayati Dk. John Pombe Magufuli.
Mshituko haukuwa mdogo kwa sababu, ni kwa mara ya kwanza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeondokewa na kiongozi wa nchi akiwa madarakani, ukiwacha kile kilichotokea visiwani Zanzibar mwaka 1972 baada ya kuuwawa kwa Rais Abeid Amani Karume.
Hivyo, matarajio ya wananchi yalikuwa makubwa pengine kuliko mabega ya Rais Samia yalivyojiandaa kuubeba mzigo alioachiwa na mtangulizi wake. Zaidi ya yote alionekana kuwa rais wa kwanza Tanzania mwenye jinsia ya kike, ubaya ni kuwa wengi wanainasibisha jinsia hiyo na udhaifu.
Siku aliyoapishwa kushika madaraka rasmi katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Rais Samia alitoa hotuba ya kukumbukwa, hotuba iliyojaa uchaguzi wa maneno, hekima na ustahamilivu wa hali ya juu. Ilibadili fikra za wengi na kuanzia hapo hakurudi nyuma.
Nikimtazama – Rais Samia ninaona vitu vitatu na pengine vingi zaidi. Ninamuona mwanadiplomasia mbobevu, ninamuona mwanasiasa mkomavu na ninamuona mlezi wa jamii iliyosahaulika; wanawake, vijana, wazee na watoto.
Kwa sababu, jamii yoyote iliyostaarabika kitu cha kwanza kukitazama ni makundi haya manne, vijana, wanawake, wazee na watoto. Ni makundi yanayokosa watetezi kwa sababu yanahitaji kutazamwa kwa jicho la karibu zaidi ya wengine ambao tayari wanajiweza.
Rais Samia Mwanasiasa
Ikumbukwe wakati akichukua nchi Machi 19, 2021 aliikuta nchi imegawanyika vipande vipande katika siasa. Vurugu na kelele za wanasiasa waliohisi kutengwa zilikuwa nyingi, mikutano ya hadhara ya wanasiasa ilizuiwa na zaidi ya yote wanasiasa hawakuwa wamepata wasaa wa kukutana na kiongozi wa nchi kwa zaidi ya miaka sita.
Sifa kubwa ya Rais Samia anaelezwa kama mwanasiasa anayependa kufanya maamuzi kupitia kusikiliza kila mmoja na si mtu wa kuamua mambo kwa pupa au kwa kuonea wengine.
Pia anaelezwa kuwa mwanasiasa jasiri na asiyeyumbishwa kwenye jambo analoliamini, hivyo kitu cha kwanza kukifanya ni kuwavuta wanasiasa wa upinzani karibu naye. Bila kujali itikadi za vyama vingi wala uana-CCM.
Ninakumbuka katika mwaka 2014 baada ya Bunge la Katiba, wakati huo Rais Samia akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira; nilikutana naye na kufanya mazungumzo ya saa moja ofisini kwake.
Nilijifunza mambo mengi kutoka kwake, wakati huo nikiwa mwandishi wa Gazeti la Raia Tanzania. Ni mtu msikivu, mwerevu na mnyenyekevu hata kwa watu asiowajua.
Alipoingia madarakani kushika nchi, Rais Samia alianza vikao vya mara kwa mara vya maofisa wa serikali na wanasiasa wa vyama vya upinzani, tukaanza kuwaona wanasiasa wakienda Ikulu kufanya mazungumzo na rais.
Hivi karibuni pia tukaona kubwa zaidi alipokuwa na ziara visiwani Pemba, alikutana na wawakilishi wa vyama vyote vya siasa visiwani humo.
Kama hiyo haitoshi, alipokuwa katika ziara zake za kikazi kama rais wa nchi alitenga muda akakutana na mwanasiasa wa upinzani Tundu Lissu nchini Ubelgiji, akafanya naye mazungumzo na kumtaka arejee nyumbani.
Awali, Rais Samia akiwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipata kwenda kumjulia hali Tundu Lisusu alipokuwa amelazwa nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi, Lissu wakati huo alikuwa Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Katika mojawapo ya matukio ya kutisha kwenye historia ya Tanzania, Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba, 2017 akiwa jijini Dodoma.
Rais Samia alikuwa ndiye kiongozi wa juu wa kwanza wa serikali – na pekee wakati huo akiwa Makamu wa Ris, kwenda kumuona mwanasiasa huyo mashuhuri.
Rais Samia Mwanadiplomasia
Tunafahamu kuwa Tanzania ni nchi pekee katika ukanda huu wa Kusini mwa Jangwa la Sahara na Afrika nzima kuwa na wanadiplomasia wabobevu, ambao wameiletea sifa Tanzania miaka na miaka.
Tukiwataja kwa uchache wapo kina Abdulrahman Babu, Salim Ahmed Salim, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, Bernard Membe na wengine wengi ambao tukiwataja hapa tutajaza gazeti.
Serikali ya Watu wa China hadi leo haiwezi kuisahau Tanzania kwa kuwatetea kurudishiwa kiti katika Umoja wa Mataifa, pia Salim Ahmed Salim mnamo mwaka 1971 wakati huo akiwa na umri wa miaka 28 tu; ndiye aliyewasaidia kuwarudishia China kiti cha UN.
Abdulrahmana Babu alikuwa na sifa kubwa katika diplomasia, ndiye aliyeiunganisha Tanzania na China pamoja na mataifa mengi ikiwemo Urusi na Ujerumani ya Mashariki. Vijana wengi walipata fursa ya kwenda kusoma nje ya nchi kupitia diplomasia zake.
Lazima tuelewe wazi kuwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, mojawapo ya eneo ambalo Serikali ya Tanzania ilikuwa imewekeza sana ni katika kutengeneza kada ya watumishi wabobezi wa masuala ya uhusiano wa kimataifa.
Nchi ilipata bahati ya kuongozwa na marais wawili; hayati Benjamin Mkapa na Kikwete ambao waliwahi kuwa Mawaziri wa Mambo ya Nje na wakiamini katika kutengeneza kada ya watumishi wanaokidhi vigezo hivyo.
Hata hivyo, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Dk. John Magufuli mambo yalibadilika, Tanzania ilipoteza marafiki wengi katika anga la kimataifa na hata diplomasia yetu iliporomoka kwa kasi ya ajabu.
Pengine tunaweza kumtetea Hayati Magufuli kwa mambo mawili au matatu, yeye hakuwahi kufanya kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje na alikuwa Rais wa kwanza wa Tanzania ambaye hakuwahi kufanya kazi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati akishughulika na wana diplomasia kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake.
Kimsingi, Magufuli alikuwa akizungumza hadharani kwamba katika kipindi cha takribani miaka 20 ya kuwa waziri katika Serikali za Mkapa na Kikwete, alisafiri si zaidi ya mara tano kwenda ughaibuni.
Kwa sababu hiyo, diplomasia yake ikawa ya kutazama ndani zaidi ya nchi yake – akipenda kutumia watu aliowaamini yeye kuliko wale waliopikwa kufanya kazi za uhusiano wa kimataifa kwa takribani miaka 20 nyuma.
Hivyo, inashangaza sana kuona Rais Samia kama alivyokuwa Rais Magufuli, hakuwahi kufanya kazi Wizara ya Mambo ya Nje wala hakuwahi kufanya kazi na Baba wa Taifa wakati akishughulika na mambo ya kidiplomasia, lakini ajabu sana mambo anayoyafanya katika anga ya diplomasia ni makubwa kuliko uzoefu wake.
Kitu muhimu na cha kipekee alichokifanya baada ya kuingia madarakani ni kumchagua Balozi Liberata Mulamulaa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, kuchukua nafasia ya Profesa Palamagamba Kabudi. Balozi Mulamula ni moja ya wanadiplomasia wabobevu nchini.
Kingine alichokifanya ni kuanza kuzungukia nchi zilizokuwa na mvutano na Tanzania, ikiwemo Kenya na mataifa ya Magharibi ikiwemo Marekani na mataifa mengine ya Ulaya.
Kote huko alirudisha taswira njema ya Tanzania na kuwaeleza dhamira yake ya dhati katika kuimarisha uchumi, kuleta utulivu wa kisiasa na zaidi ya yote kuwahudumia Watanzania kwa uwezo wake wote.
Misaada iliyofunga ikaanza kufunguka, mikopo iliyokwama ikaanza kukwamuliwa na vinyongo vilivyofunga kwa majirani zetu hasa Kenya, vikaanza kufunguliwa.
Rais Samia Mlezi wa Jamii
Kama nilivyoeleza awali, sifa kubwa ya Rais Samia ni upole, unyenyekevu, usikivu na huruma kwa jamii anayoiongoza. Ingawa anakuwa mkali yanapoguswa maslahi ya nchi.
Hivyo, hatua ya kwanza kuifanya baada ya kuingia madaraani ni kuruhusu mabinti wote waliofukuzwa shuleni kwa sababu mbalimbali ikiwemo kupata ujauzito warejeshwe darasani.
Pili akaongeza kiwango cha mkopo wa elimu ya juu kutoka Shilingi Bilioni 500 hadi Bil 570/-ambazo zitawanufaisha zaidi ya wanafunzi 160,000. Hii maana yake anataka watoto zaidi wasome ili jamii iwe na wasomi.
Tatu akaongeza wigo wa elimu bure, awali ilikuwa inaishia kidato cha nne, yeye akapeleka hadi kidato cha sita. Maana yake mwanafunzi anayetoka familia duni anao uwezo wa kusoma kuanzia darasa la awali hadi chuo kikuu kwa fdha za serikali. Maana yake, atasoma hadi kidato cha sita bila malipo na akifika chuo kikuu anapata mkopo ambao ataurejesha akianza kufanya kazi.
Vilevile, alitangaza na kusisitiza matibahu na maslahi ya wastaafu yazingatiwe, akaongeza kimaa cha mishahara kwa watumishi wa umma na akafanya kubwa zaidi, kuongeza posho za kujikimu kwa watumishi wa umma wawapo nje ya vituo vya kazi.
Nani kama Mama?

hafidhkido@yahoo.com

About the author

mzalendoeditor