Featured Kitaifa

WAZIRI MKENDA:’WATANZANIA TUMIENI KISWAHILI FASAHA’

Written by mzalendoeditor

Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dar es Salaam

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema watanzania lazima waenzi na kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha.

Waziri Prof. Mkenda amesema hayo Julai 5, 2022 jijini Dar es Salaam  alipokuwa Mgeni Rasmi katika Mdahalo kuhusu Lugha ya Kiswahili na Elimu ambayo ni sehemu ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani Julai 7, 2022.

“Roho ya nchi ni utamaduni wake, sisi Watanzania ni lazima tuwe mstari wa mbele kuhakikisha tunaongea Kiswahili fasaha, hili ni jukumu letu. BAKITA na BAKIZA muwe mstari wa mbele ili kukuza na kuendeleza matumizi ya Kiswahili na istilahi za Kiswahili” amesema Prof. Mkenda.

Katika kuhakikisha Kiswahili fasaha kinatumika, Prof. Mkenda amesema Wizara yake itaendelea kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Barazala Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Braza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) katika kusukuma mbele masuala ya filamu ili kusaidia kukuza na kueneza Kiswahili ndani na nje ya nchi.

Waziri Prof. Mkenda ametumia fursa hiyo kuhimiza uandishi wa mashairi, riwaya, tamthilia pamoja na hadithi ili kusaidia kukuza lugha ya Kiswahili.

“Angalieni fursa za Kiswahili nje ya Tanzania, ukisoma Kiswahili, ni ‘dili’ na kitakupeleka ng’ambo, tunahitaji walimu wenye ufasaha katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza na uwezo mzuri wa kufundisha” amesema Prof. Mkenda.

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani hapa nchini yatafanyika Julai 7, 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ambapo dunia nzima itasherehekea siku hiyo kwa mara ya kwanza baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kutangaza rasmi Julai 7 ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.  

 

About the author

mzalendoeditor