Featured Kitaifa

WATAALAM WA UJENZI WAKUTANA KUJADILI USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA BARABARA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza na watalaam na wadau wa Sekta ya Ujenzi (hawapo pichani), katika semina elekezi ya utunzaji wa rasilimali za barabara inayofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC, Mkoani Arusha. Semina hiyo imeandaliwa na Chama cha Barabara Tanzania (TARA).

Mwenyekiti wa Chama cha Barabara Tanzania (TARA), Bw. Joseph Haule, akitoa taarifa ya Chama hicho katika semina elekezi iliyowakutanisha wataalam na wadau wa Sekta ya Ujenzi kujadiliana namna bora ya kuzisimamia na kuzikarabati barabara, mkoani Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, akiwakaribisha wataalam wa Sekta ya Ujenzi (hawapo pichani), ambao wamekutana mkoani humo katika semina elekezi ya utunzaji wa rasilimali za barabara.

Baadhi ya wataalam na wadau wa Sekta ya Ujenzi wakisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani), katika semeni elekezi kwa ajili ya utunzaji wa rasilimali za barabara, mkoani Arusha.

PICHA NA WUU

……………………………………….

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amefungua semina ya kikanda kwa Watalaam wa Sekta ya Ujenzi ambao wamekutana na kujadiliana taratibu na mpango wa kisasa wa jinsi ya kusimamia, kuzilinda na kuzikarabati rasilimali za barabara zilizokwishakamilika na zile zinazoendelea kujengwa hapa nchini.

Semina hiyo ya siku tano (5) inayofanyika mkoani Arusha katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC imeandaliwa na Chama cha Barabara Tanzania (TARA) na imehusisha wataalamu kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB).

Waziri Prof. Mbarawa amesema kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya barabara hapa nchini ambapo kwa sasa inakadiriwa thamani yake ni takribani dola za kimarekani bilioni 15 hivyo ni wakati sasa wa kupata utaratibu mzuri utakaotuwezesha kujua rasilimali ziko wapi, zinasimamiwaje na zinaendelezajwe kwa kuwa zina gharimu kiasi kikubwa cha fedha.

“Kawaida tunajenga barabara lakini mwisho wa siku zinakosa usimamizi, angalizi na matengenezo lakini kupitia mkutano huu wataalam wetu sasa wataongeza uwezo wa kuzisimamia barabara zetu na kuzitengeneza kwa wakati”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa malengo ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanaweza kunufaika na miundombinu bora ya barabara bila ya kuleta athari yoyote na hivyo kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.

Naye, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Rogatus Mativila, ameeleza kuwa Wakala umejipanga vyema kuendelea kujenga barabara kwa viwango lakini pia kuzisimamia na kuzifanyia matenegenezo kwa wakati pindi zinapohitajika ili ziweze kudumu kwa kipindi kirefu.

“Tunaimaini baada ya semina hii kutakuwa na mabadiliko makubwa ya utunzaji wa barabara kwa kile tulichojifunza hapa tutakwenda kukitekeleza na kuwa na miundombinu bora ya barabara hapa nchini”, amefafanua Eng. Mativila.

About the author

mzalendoeditor