Featured Michezo

WAZIRI MCHENGERWA ATAJA MAKUBWA YA RAIS SAMIA KATIKA MICHEZO,AZINDUA MBIO ZA CRDB MARATHON AJISAJILI

Written by mzalendoeditor


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa akizungumza wakati wa halfa ya uzinduzi huo

Na John Mapepele.
Waziri
wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan
imekua mstari wa mbele siyo tu katika  kuweka mazingira mazuri ya
uwekezaji katika michezo  bali inashiriki moja kwa moja kuwekeza katika
michezo kwa  kuwa inaamini kuwa michezo ni uchumi na biashara ambayo
inatoa ajira nyingi kwa vijana.
 Mhe.
Mchengerwa amesema hayo leo Mei 5, 2022 kwenye uzinduzi wa msimu wa
tatu wa mbio za kimataifa za CRDB kwenye viunga vya Nyerere jijini
Dodoma ambapo amewataka wakuu wote wa mikoa na wilaya nchi nzima
kuhamasisha michezo kwenye maeneo yao ili kusaidia wananchi kujenga
afya, kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kuinua uchumi wao na taifa
kwa ujumla. 
Aidha,
amewaelekeza maafisa michezo na utamaduni katika kila mkoa na wilaya
kuratibu mazoezi na mashindano ya michezo na sanaa ili kubaini na
kuwatambua watanzania wenye vipaji kupitia program iliyoanzishwa na
Serikali ijulikanayo kama mtaa kwa mtaa ili kuwanyanyua wafike kwenye
kiwango cha kimataifa, ambapo amesema tayari Serikali  imetenga fedha 
kwa ajili ya kazi hiyo. 
 “Katika
kipindi cha mwaka mmoja tangu aingie madarakani, Mhe. Rais  Samia
ameweka misingi, na mikakati iliyojikita katika masuala kadhaa ya muhimu
ikiwemo nyongeza ya bajeti ya Wizara, punguzo au kuondolewa kwa kodi ya
nyasi bandia ili kuimarisha viwanja vya soka pamoja na kuanzishwa kwa
mfuko wa maendeleo ya michezo nchini. 
 Mfuko
huo umepewa chanzo madhubuti ambacho ni fedha za asilimia tano 5% ya
mapato yatokanayo na michezo ya kubashiri matokeo ya michezo (Sports
Betting)” amesisitiza Mhe Mchengerwa.
Amefafanua
kuwa, Mhe. Samia  ameelekeza kuwa mfuko huo ukasaidie shughuli
mbalimbali za michezo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha timu za Taifa
zinahudumiwa na kuratibiwa ipasavyo, miundombinu ya michezo inaboreshwa
na kujengwa, wataalamu wa michezo wanapewa mafunzo yanayostahili ikiwa
ni pamoja na makocha ili kuendana na hali halisi halisi Duniani. 
Kwa
upande wa sekta za Utamaduni na Sanaa amefafanua kuwa kwa mara ya
kwanza katika historia ya sanaa, mwaka huu wasanii  wameanza kunufaika
kwa kupokea mirabaha kutokana na kazi zao za sanaa, ambapo amesema
kumekuwa  changamoto chache ambazo zinafanyiwa kazi sambamba na
kuzingatia maelekezo aliyoyatoa Mhe. Rais Mei 31 mwaka huu wakati wa
uzinduzi wa Tamasha la Muziki wa Hiphop la “The Dream Concent” Jijini
Dar es Salaam. 
Amesisitiza
kuwa tayari Serikali imeanza ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kuja
kuratibu mashindano ya kimataifa hususan mashindano ya Kombe la Mataifa
ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027 ambapo amewaomba wadau mbalimbali ikiwa
ni pamoja na CRDB kushirikiana na Serikali katika kujenga  miundombinu.
 “Kama
Wizara tumejipanga kuhakikisha ndoto za Mhe. Rais Samia na watanzania
kwenye michezo zinatimia kwa sisi kufanya vizuri, nimeshawambia wenzangu
kuwa mimi kama Waziri mwenye dhamana sitakubali  kupokea sababu zisizo
na msingi kuhusu kwa nini tunafanya vibaya kwenye michezo ”amesisitiza,
Mhe. Mchengerwa. 
Pia
amesema Serikali imerejesha Tuzo kubwa kabisa za Filamu pamoja na
Muziki Tanzania zilizofanyika Disemba, 2021 na mwanzoni mwa mwezi Aprili
2022 ambapo amesisitiza kuwa kurejea kwa tuzo hizo kunatoa hamasa kwa
wasanii kuendelea kutoa kazi zenye ubora zaidi ambazo pamoja na
kuwaingizia kipato zitachangia kutangaza nchi yetu katika ngazi ya
kimataifa.
 Aidha
amewahimiza wanamichezo na wadau wa michezo wote kwa kujitokeza kwa
wingi katika zoezi la sensa ya watu na makazi, litakalofanyika tarehe 23
Agosti, 2022.
Katika uzinduzi  huo amekuwa mtu wa kwanza kujisajili kukimbia kilomita 42.

About the author

mzalendoeditor