Featured Kitaifa

BARABARA YA MVUMI KUWEKWA LAMI KM 3

Written by mzalendoeditor

Asila Twaha , TAMISEMI

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. David Silinde amesema, Serikali inaendelea kutafuta rasilimali ili barabara ya mvumi Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma ijengwe kwa kiwango kwa Lami kwa urefu wa km tatu.

Mhe. Silinde ameyasema hayo leo Mei 25, 2022 wakati wa ziara yake ya kukagua barabara iliyojengwa kwa kiwango cha lami kilometa 1 kuanzia eneo la makaburini hadi bilia kata ya mvumi mission Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Jijini Dodoma.

Wakati wa ziara hiyo Mbunge wa Jimbo la Mvumi Mhe. Livingstone Lusinde aliwasilisha ombi la wananchi wake kutaka kuongezewa barabara ya lami ili kuongeza hadhi ya Kata hiyo na kurahisisha shughuli za usafirishaji.

Mhe. Silinde amesema suala hilo litafanyiwa kazi na atahakikisha anasimamia utekelezaji kwa vitendo ili barabara hiyo ipate lami ya kutosha kuipa hadhi Mvumi kuwa mji mdogo.

“Tuendelee kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na kumuunga mkono ili aweze kufanya mambo makubwa zaidi kama mnavyoona kwenye utekelezaji wa miradi na sisi wasimamizi wake tutaendelea kuisimamia kwa vitendo niwahakikishie mvumi mtaongezewa lami zaidi ya kilomita 2.

Aidha Mhe. Silinde amesema ameridhishwa na ukaguzi aliofanya katika barabara hiyo kwa kuwa asilimia kubwa umekamilika na amemuelekeza Meneja Wakala wa Barabara za Mjini na Vjijini TARURA kuandaa bajeti ya uwekaji wa taa za kwenye barabara hiyo .

“Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ametuagiza sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunapojenga barabara tuweka na taa za barabarani niwaelekeze TARURA hili tutalisimamia” amesema Mhe. Silinde

Naye Mbunge wa Jimbo la Mvumi Mhe. Livingstone Lusinde, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Rais –TAMISEMI kwa kuhakikisha wanaisimamia TARURA kwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara na ameishukuru Serikali kuridhia ombi la wananchi kuongezewa kilomita za lami.

“Sisi wananchi wa mvumi pamoja na maendeleo tunayo yaona Serikali inayofanya lakini pia tumejiandaa kwa ajili ya zoezi la sensa kuhesabiwa linalotegemewa kuanza nchi nzima mwezi Agosti,2022 na niombe Serikali iendelee kutuunga mkono kuleta maendeleo hapa Mvumi ” amesema Mhe. Lusinde

About the author

mzalendoeditor