Featured Kitaifa

WATAALAMU WA UANDISHI WA VITABU VYA KIADA WAHIMIZWA KUTUMIA UWEZO WAO KUANDIKA VITABU VILIVYOBORA

Written by mzalendoeditor

  

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amewahimiza wataalamu wa uandishi wa vitabu vya kiada kutumia uwezo wao wote ili waweze kuandika vitabu bora kwa ajili ya maslahi ya taifa.

Ameyasema hayo leo tarehe 21/04/ 2022 kwenye ufunguzj wa kazi ya Uhariri wa Maudhui wa aina 43 za  visawidi vya vitabu vya kiada kidato cha kwanza hadi cha sitana uhariri wa lugha viongozi vitano vya walimu vya darasa la tano uliofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Morogoro Mjini.

“Wataalamu ninawaomba sana mtumie uwezo na uzoefu wenu wote katika kuifanya kazi hii ya uhariri ili kuwezesha kupatikana vitabu ambavyo vitakuwa bora ” amesema Dkt. Komba

Ameeleza pia uhariri huo unahitaji kufanyika kwa uaminifu mkubwa kwa muda wote na haipaswi kabisa mtaalamu yoyote kusambaza nakala yoyote nje ya kikao kazi husika.

Pamoja na mambo mengine , amewataka wataalamu kuwa huru katika uhariri wao, na kama kuna sehemu itahitajika kubadilishwa kwa kuongeza ama kupunguza  jambo hata kama halipo kwenye mhtasari ilimradi viendane na maendeleo ya teknolojia, ifanyike ivyo ili kukidhi lengo la ujifunzaji.

Pia amesema wakati wa uhariri wataalamu wakubaliane juu ya maboresho yoyote badala ya Kila mtaalamu kuboresha kitu kulingana na upenzi wake binafsi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ubunifu na uboreshaji wa vifaa vya kielimu Bwana Fixon Mtelesi amewasihi watalaamu kutumia lugha iliyorahisi na yakueleweka kwa wanafunzi kulingana na kiwango chao cha elimu lakini pia maudhui na mifano iliyomo kwenye vitabu hivyo isadifu mazingira halisi ya wanafunzi.

Taasisi ya Elimu Tanzania inatarajia kukamilisha zoezi la uandishi wa vitabu vya kiada ndani ya mwezi wa sita 2022.

About the author

mzalendoeditor