Featured Kitaifa

WALIMU WA VYUO VYA UFUNDI KUANZA KUFUNDISHA KWA NJIA YA MTANDAO.

Written by mzalendoeditor

Kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Uviko 19 Serikali imeshauriwa kuweka mazingira rafiki ya kufundishia kwa njia ya masafa mrefu (kwa njia ya mtandao) kwa walimu wa vyuo vya mafunzo na ufundi stadi hapa nchini kwa kununua vitendea kazi vitakavyo wasaidia walimu kufundisha wakiwa popote lengo likiwa ni kupunguza maapukizi ya ugonjwa huo.

Hayo yameelezwa na baadhi ya walimu wa vyuo vya ufundi stadi hapa nchini walipokutana Mjini Morogoro kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo ya namna ya kufundisha kwa njia ya mtandao yalioandaliwa na Shirika Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kupitia mradi wake wa Better Education for Africa Rise II.

Wamesema kutokana na changamoto mbalimbali zinazoikumba Sekta ya hapa nchini ikiwemo changamoto ya ugonjwa wa Uviko 19 kuna haja Serikali kushirikiana na wadau wa elimu Ikiwemo UNESCO kuwekeza kwenye vitendea kazi vya kufundishia kwa njia ya mtandao kwani elimu ya masafa itawasaidia wanafunzi kuendelea na masomo hata pale zinapotokea changamoto zikiwemo za magonjwa ya mlipuko.

“Tunaishukuru UNESCO kwa kutupatia mafunzo haya kwani yatatusaidia kufundisha wanafunzi wengi zaidi kwa wakati mmoja bila ya kukutana nao, pia mihula ya masomo yao haitovulugika hata kama yatatokea majanga.” Walisema walimu hao.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo Kaimu Mkuu wa chuo cha Walimu wa ufundi stadi Morogoro Bwana Andrew Boi amesema kuna uhuhimu wa kufundisha kwa njia ya mtandao katika vyuo vya mafunzo na ufundi stadi huku akiiomba  UNESCO kuendelea kushirikiana na Serikali ili vyuo vyote hapa nchini viweze kutoa elimu kwa njia ya mtandao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Wizara ya Elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi  Daktari Noel Mbonde amesema  elimu ya masafa itawapa fursa walimu kufundisha wakiwa popote bila  hata kuingia darasani na kupunguza  msongamano usiokuwa wa lazima maeneo ya vyuo hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana na ugonjwa wa uviko 19.

“Hakuna ulazima wa mwalimu kwenda darasani na kuanza kufundisha unaweza kukaa ofisini kwako  ukafundisha na wanafunzi wakapata elimu kama kawaida.” alisema Dakta Mbonde 

Aidha amewataka walimu hao waliopata mafunzo kuwa mabalozi wazuri katika vyuo vyao ili kuendana na ukuaji wa teknolojia na kupambana na majanga mbalimbali yakiwemo ya magonjwa ya mlipuko ukiwemo UVIKO 19.

Mradi wa Better Education for Africa Rise II ni Mradi wa miaka mitano unaotekelezwa  na Shirika Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) umeanza mwaka 2017 na kumalizika mwaka 2022 na kuwafikia walimu kutoka vyuo mbalimbali vya mafunzo na ufundi stadi hapa nchini.   

 

About the author

mzalendoeditor