Featured Kitaifa

MFANYABIASHARA ADAIWA KUBAKA NA KULAWITI WATOTO WATATU

Written by mzalendoeditor

JESHI la Polisi mkoani Geita linamtafuta mkazi wa Kijiji cha Bukori (jina limehifadhiwa), kwa tuhuma za kuwabaka na kuwalawiti watoto watatu wa darasa la tatu wa familia moja wa Shule ya Msingi Bukori.

Wanafunzi hao wameumizwa sehemu zao za siri kiasi cha kushindwa kwenda haja. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe, alisema tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Bukori wilayani Geita, alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa mtuhumiwa huyo (jina limehifadhiwa) ni mwanafamilia hiyo.

Alisema ukatili waliofanyiwa watoto hao ni ndani ya familia na jamii ambao ulibainika baada ya watoto kushindwa kujisaidia aja zote kutokana na maumivu.

“Ukatili mbaya sana upo ndani ya familia, kuna kesi pale Bukori upelelezi bado unaendelea, ndani ya familia kuna mtu mfanyabiashara sijui yuko wapi, kila akija anawaingilia watoto na kuwaambia wasiseme, na kwenye familia hiyo mtuhumiwa huyo yeye ndiye mwenye uwezo wa kifedha anawapatia fedha za chumvi,” alisema na kuongeza:

“Kuna watoto watatu anawafanyia ukatili wa kingono, siku ya kugundulika kwa tukio hilo mwanafunzi mmoja aliingia chooni kujisaidia katika Shule ya Msingi Bukori akashindwa kutoka kwa kuwa sehemu ya haja kubwa ilikuwa imeharibika na wanafunzi wenzake walikuwa wakipiga kelele mbona hautoki chooni ili waingie, hadi mwalimu alipofika akaingia akakuta mwanafunzi huyo akiwa kwenye maumivu makali.”

Alisema: “Mwalimu alimpeleka mwanafunzi huyo Kituo cha Afya Bukori, alipohojiwa alimtaja anayewafanyia vitendo hivyo ni ndugu yao anayekuja mara kwa mara, alieleza pia siyo peke yake bali kuna wengine wawili wamefanyiwa kama yeye.”

Kwa mujibu wa Mwaibambe, ngazi ya familia ndiyo kuna ukatili mwingi, lakini inakuwa ni ngumu kwa polisi kupata taarifa, na kwamba wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo ambalo walijua baada ya mwanafunzi huyo kuanguka chooni.

“Kitendo alichokifanya mtuhumiwa huyo ni cha kikatili sana, sisi polisi tunamtafuta kwa sababu ni mwanafamilia tutampata tu na tukimkamata tutampeleka mahakamani, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake,” alisema na kuongeza:

“Wazazi na walezi jitahidini kuwakagua watoto wenu wa kike na wa kiume ili kugungua kama wamefanyiwa ukatili wa kingono, mnahangaikia na biashara zenu tu pamoja na VIKOBA hamwangalii maendeleo ya watoto wenu.”

Aidha, Kamanda Mwaibambe aliwatahadharisha wananchi wa mkoa huo kuwa wamebaini usafiri wa bajaji ni hatarishi kwa kuwa kuna matukio ya ukatili wa kijinsia na uhalifu mwingine.

CHANZO:GLOBAL TV

About the author

mzalendoeditor