Na. John Mapepele
Mkuu wa Dodoma. Mhe, Antony Mtaka amesema tamasha kubwa la kihistoria la Muziki la Serengeti linaloratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na wadau litakalofanyika jijini Dodoma Machi 12-13, 2022 ni fursa pekee ya kiuchumi kwa wakazi wa Dodoma na nchi nzima kwa ujumla.
Mhe. Mataka ameyasema haya leo Machi 4, 2022 ofisini kwake ambapo amefafanua kwamba tamasha hilo linatarajia kuwakutanisha zaidi ya wasanii mia moja wa muziki ambao watakuwa na mahitaji mbalimbali hivyo wakazi wa Dodoma watanufaika kwa kuwauzia bidhaa.
“Tunaishukuru Serikali yetu kwa kutusogezea wimbi la wasanii zaidi ya mia moja kwa mara moja kwa kuwa tunakwenda kunufaika sana. Huu ni utalii wa kiutamaduni na kiuchumi, shime wanadodoma tutumie fursa hii adimu”. Ameongeza Mhe. Mtaka
Aidha, Mhe. Mtaka ameipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ubunifu wa kuongeza siku ambapo sasa litafanyika kwa siku mbili badala ya moja kama ilivyopangwa awali kutokana na mahitaji makubwa ya tamasha hilo kwa wasanii na wananchi.
Ametoa wito kwa wananchi wote wa Dodoma kushiriki kikamilifu kwenye tamasha hili la kihistoria na kuwaomba wasanii wa Dodoma kutumia tamasha hili kujifunza ili waweze kupiga hatua zaidi katika kazi zao.
“Wasanii wa Dodoma jitokezeni kwa wingi ili kujifunza na kupata uzoefu kutoka kwa wanamuziki na wasanii wakongwe watakaotumbuiza kwenye tamasha hilo”. Amesisitiza Mhe. Mtaka
Kwa upande wake, Dkt. Abbasi amesema kuwa Tamasha hili ndiyo tamasha pekee kubwa linalowaleta pamoja wasanii mbalimbali, wachanga na wakongwe, pia bendi za muziki kujumuika pamoja bila kujali lebo zao.
Ameeleza kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha wasanii wanabadilishana uzoefu kwenye fani ya muziki ili kukuza vipaji vyao huku wakitumia tamasha hilo kutangaza utalii na vivutio mbalimbali vya Tanzania sasa inakwenda kufikiwa kwa ukamilifu.