Featured Kitaifa

WAZAZI TAMBUENI MAHITAJI YA WANAFUNZI- RC RUKWA

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akikagua moja ya darasa wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika shule ya msingi Kisumba iliyopo Manispaa ya Sumbawanga juzi ambapo alitoa zawadi ya sare kwa wanafunzi wahitaji.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Kisumba juzi alipotembelea kukagua miundombinu ya shule.Shule hiyo ina wanafunzi 988 huku ikiwa na walimu 10 na upungufu ikiwa ni walimu 12 .

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Kisumba walipatiwa zawadi ya sare na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (aliyesimama kulia) juzi alipotembelea shule hiyo iliyopo Manispaa ya Sumbwanga.

Katibu Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Daniel Noah akigawa zawadi ya sare kwa wanafunzi wa shule ya msingi Kisumba juzi ambapo jumla ya wanafunzi 50 walipatiwa mashati mapya na Mkuu wa Mkoa huo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akisaini kitabu cha wageni juzi alipofanya ziara ya kushtukiza katika shule ya msingi Kisumba wilayani Sumbawanga kukagua ufundishaji na miundombinu. Kulia ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Frank Kasunga.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa

………………………………………………………

Na. OMM Rukwa

Wazazi na walezi wa watoto katika mkoa wa Rukwa wamekumbushwa wajibu wao wa msingi kwa malezi  ikiwemo upatikanaji wa chakula, malazi na chakula bora ili watoto waweze kusoma vema.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti  wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika shule ya msingi Kisumba iliyopo Manispaa ya Sumbawanga kukagua mwenendo wa usomaji na ufundishaji.

Akiwa katika shule hiyo yenye wanafunzi 988 wa darasa la awali hadi la saba  huku ikiwa na walimu kumi (10) kati ya mahitaji ya walimu 22, Mkuu huyo wa Mkoa alijionea msongamano uliopo kwenye baadhi ya madarasa ya shule hiyo.

“Nimejionea mazingira yenu ya ufundishaji hapa .Bado kuna msongamano hususan darasa la pili na la tatu watoto ni wengi huku kukiwa na upungufu mkubwa wa walimu hatua inayoweza athiri ufundishaji wa wanafunzi. Tutatafuta ufumbuzi haraka” alisema Mkirikiti.

Katika hatua nyingine Mkirikiti alitoa zawadi ya mashati mapya kwa wanafunzi Hamsini (50) ambao alibaini kuwa na uhitaji mkubwa wa sare shuleni hapo.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ya Kisumba Frank Kasunga alishukuru kwa kutembelewa na Mkuu wa Mkoa ambapo alisema wamefarijika kupata ugeni huo.

“Tunashukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuja kututia moyo ambapo umejionea mazingira yetu ya kazi, tunaomba tusaidiwe kupata walimu ili tuweze kukidhi malengo ya ufundishaji kutokana na wingi wa wanafunzi” alisema Kasunga.

Kasunga aliongeza kusema anamshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kugawa sare kwa wanafunzi wahitaji kwani hilo ni jukumu la wazazi lakini imekuwa mfano mzuri kwa jamii kutoa msaada kwa wahitaji.

Nao wanafunzi Estoni Ngua na Apoliana Selewi wa darasa la saba walimshukuru kumuona Mkuu huyo wa Mkoa pia kuwapa zawadi wenzao.

Mkuu huyo wa Mkoa alifanya ziara hiyo ya kushtukiza kujionea hali halisi ya ufundishaji kwenye shule za msingi ikiwa ni pamoja na kukagua miundombinu ya madarasa.

About the author

mzalendoeditor