Featured Kitaifa

MAJALIWA AZUNGUMZA NA VIONGOZI WA TARAFA YA NGORONGORO

Written by mzalendoeditor

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi alipowasili kwenye viwanja vya ukumbi wa Ngorongoro mkoani Arusha kuzungumza na  viongozi na mwananchi wa Tarafa hiyo

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro, katika ukumbi wa mikutano wa Ngorongoro Mkoani Arusha

Baadhi ya viongozi na wawakilishi wa wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipozungumza nao Mkoani Arusha  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 

.…………………………………………………………….

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imepokea kauli ya wakazi wa Ngorongoro kwamba wako tayari kupokea maelekezo ya Serikali na kushirikiana pamoja katika kuulinda utalii na uhifadhi wa eneo hilo.

“Kwa kauli yenu kwamba mko tayari kushirikiana na Serikali kuendeleza uhifadhi na kukuza utalii, sisi tumeipokea na tutaitekeleza ahadi yenu”

Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo leo jioni (Alhamisi, Februari 17, 2022) wakati akizungumza na viongozi na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro kwenye kikao cha ndani kilichofanyika makao makuu ya zamani ya NCAA, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha.

Amesema, kama ambavyo Serikali imetoa nafasi ya kusikiliza maoni ya wananchi wa tarafa hiyo, nao hawana budi kuipa nafasi Serikali kuendelea na mpango wa maboresho wa maeneo ambayo yanatakiwa kufanyiwa uhakiki ili ije na mpango bora wa kuliendeleza eneo hilo.

Amesema atapitia changamoto alizokabidhiwa na Diwani wa Naiseko, Bw. James Moringe na akawataka wakazi hao waendelee kuiamini Serikali yao kwa sababu ina nia njema na wananchi wake.

“Endeleeni kuiamini Serikali yenu kwani ina njema na nyie. Tunahitaji kuona shughuli za ufugaji zikiendelea na utalii ukiendelea. Na kwa maana hiyo, mnakubaliana na Watanzania wanaotaka kuona utalii ukiendelea. Na kwa maana hiyo tufuate misingi ya uhifadhi.”

“Na mnapotoka hapa, kila mmoja wetu akatafakari kuhusu changamoto ya kuongezeka kwa mifugo na idadi ya watu. Muwe watulivu wakati Serikali ikifanyia kazi maoni yenu. Tutapokea pia maoni ya taasisi na asasi za kiraia, nazo pia tutazifanyia kazi,” amesisitiza.

Amesema Serikali itaratibu maoni yanayotolewa na pande zote. “Tunapofanya hilo, mahali pote tunaangalia maslahi ya Taifa. Wana-Ngorongoro endeleeni kuiamini Serikali yenu,  endeleeni kumuamini Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu na endeleeni kuamini miongozo inayotolewa kwani ina tija kwenu.”

“Wakati wote Mheshimiwa Rais amesema anawapenda Watanzania wake na ni kweli anatupenda sana. Yeye ndiye mtumishi nambari moja na sisi ni wasaidizi wake na ni lazima tufuate philosophy yake ambayo anataka kuona Watanzania wanasikilizwa na wanashauriwa.”

Waziri Mkuu amesema muendelezo wa vikao anavyofanya katika wilaya ya Ngorongoro ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwataka viongozi wakutane na wakazi hao na kuwasikiliza maoni yao.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI, Naibu Waziri wa Ardhi, Makatibu Wakuu wa wizara za Maji na TAMISEMI na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wa dini.

Wadau walioshiriki kikao ni Mbunge wa Ngorongoro, Malaigwanan, Wenyeviti wa vijiji na Vitongoji, Baraza la Wafugaji la Ngorongoro, viongozi.

About the author

mzalendoeditor